OPERESHENI ya kuwaondoa wadaiwa sugu wa Wakala wa Nyumba Tanzania (TBA) mkoani Pwani, inaanza Februari 19, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya mkakati unaoendeshwa nchi nzima kwa wadaiwa 432,wanaodaiwa jumla ya Sh bilioni 7.3.
Akizungumzia operesheni hiyo, jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Kutoa wadaiwa sugu wa TBA, Gilbert Mwasambo alisema kazi hiyo itaanza Ijumaa wiki ijayo baada ya wao kukamilisha taratibu zote.
Alisema operesheni hiyo itaanza Bagamoyo kisha itaendelea mjini Kibaha kabla ya kuhamia Kibiti ambako wapangaji hao wanadaiwa zaidi ya Sh milioni 48.
Awali operesheni kama hiyo ilianzia mkoani Kigoma, kisha kuingia Dar es Salaam wiki iliyopita na katika eneo la Wazo Hill lililokuwa na wadaiwa sugu 220 waliokuwa wakidaiwa Sh Bilioni 1.6 wameingia mkataba wa makubaliano na TBA ya kuanza kulipa madeni hayo kidogo kidogo kwa muda wa miezi mitano kuanzia sasa.
Mwasambo alisema hatua huyo ilifikiwa baada ya operesheni ya kuwatoa wadaiwa hao kuanza na wakati wakiendelea nalo, wadaiwa hao waliomba kutafuta suluhu kwa njia ya mazungumzo.