Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Operesheni ya DC Mtatiro yawanasa 11, atoa onyo

85729 Pic+mtatiro Operesheni ya DC Mtatiro yawanasa 11, atoa onyo

Mon, 25 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Polisi wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania linawashikilia makarani na waandishi 11 wa vyama vya msingi kwa tuhuma za kununua korosho za wakulima kwa fedha taslimu katika vituo vya kukusanyia korosho kisha kuziingiza kwenye mfumo rasmi wa stakabadhi ghalani.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na operesheni maalumu ya kupambana na biashara haramu ya korosho maarufu ‘Kingomba’ iliyoendeshwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro.

Mbali na kuwakamata watumishi hao, Mtatiro amewasimamisha majukumu hayo na kuwapiga marufuku kujihusisha na masuala ya korosho kwenye vyama vya msingi katika msimu huu na kuwataka viongozi wa vyama wanavyotoka watuhumiwa wawaondoe kazini kuanzia leo Jumatatu.

"Wamekuwa wakiwashinikiza wakulima wawaachie korosho zao kisha mnawalipa fedha taslimu Sh1,500 kwa kilo moja na kisha korosho hizo mmekuwa mkiziingiza kwenye mfumo rasmi kwa kutumia majina ya matajiri waliowakabidhi fedha ili kufanya uhuni huo," amesema Mtatiro

Akizungumza leo Jumapili Novemba 24, 2019 katika kikao chake na viongozi,  waandishi na makarani wa vyama vya msingi wapatao 500  wilayani Tunduru amesisitiza operesheni kangomba itakuwa endelevu.

Amesema siyo tu watuhumiwa hao wameripotiwa bali hata korosho za mtego zilipowafikia walizinunua ndipo alipobaini ni vinara wa kuvunja viapo vyao vya kazi kwenye vyama vya msingi.

"Nawahakikishia kuwa, ikiwa mtaendelea kujihusisha na mchezo huu wa hovyo, sitasita kuchukua hatua zilezile; kuwakamata, kuwaondoa kwenye shughuli za Amcos na kuwashtaki,” amesema.

Hata hivyo, amemuagiza Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) kuhakikisha kinakuwa na orodha ya vijana wengi waliohitimu kidato cha nne ili waweze kuchukua nafasi za makarani na waandishi wasio waaminifu zoezi la kuwabaini na litaendelea msimu mzima wa korosho.

Chanzo: mwananchi.co.tz