Dodoma. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameagiza watumishi wanne walikuwa katika kituo cha ukaguzi wa mifugo cha Kibaha kuondolewa mara moja kituoni hapo na kupangiwa sehemu nyingine baada ya kudhibitika kuwa utendaji wao ni si mzuri.
Akizungumza leo Jumanne Desemba 4, 2018 wakati wa tathimini ya operesheni Nzagamba inayohusiana na sekta ya mifugo, Mpina amesema ni vyema watendaji wabovu wakaondolewa katika maeneo hayo.
“Watendaji walio katika kituo cha Kibaha kutokana na udhaifu mkubwa wa usimamizi wa shughuli zao waondolewe leo na kuteuliwa wengine. Kesho wawepo wengine wa kuiwakilisha wizara katika eneo hilo,” amesema.
Mpina pia ameagiza kuhamishiwa wizarani kwa watumishi wawili wa halmashauri waliofanya vizuri katika operesheni ya kwanza na ya pili ili waweze kutumikia nchi nzima katika shughuli za uvuvi.
Maagizo mengine ni kupunguza urasimu wa maeneo ya kutoa vibali vya mifugo inayokwenda nje ya nchi, kuongeza vituo tisa vya ukaguzi wa mifugo ili kuzuia utoroshaji wa mifugo.
Mpina pia aliagiza kuanzisha kanda ya usimamizi nchini ili kuongeza usimamizi wa mifugo nchini katika minada.
Kwa upande wake naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema bado watu wengi ni wazito katika kufuata sheria na taratibu.
“Kama tusingefanya jitihada hizi mambo ya uholela yangeendelea kwa hiyo jitihada hizi zimetusaidia katika kuwatoa watu katika uholela na kuonyesha nchi yetu inazo sheria na taratibu zake,” amesema.
Amesema kupungua kwa faini walizokuwa wanatoza katika operesheni hiyo kunaonyesha kuwa wadau wao wameelewa juu ya utii wa sheria.