TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kilimanjaro, imewataka viongozi wa serikali za mitaa kutoruhusu mtu ama taasisi kupitisha fedha zisizo na uhalali katika akaunti zao.
Imesema kutumia fedha hizo kwa matumizi yoyote halali ikiwemo kujenga nyumba, ununuzi wa gari, kulipa ada au matibabu ni kufanya kosa la utakatishaji wa fedha hizo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Frida Wekesi alisema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu athari za rushwa kwa viongozi wa serikali za mitaa pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi za shina na kata.
Katika semina hiyo iliyohusisha viongozi wa vijiji na kata katika Jimbo la Same Magharibi, Wekesi alitaka viongozi hao kuepuka mtego huo kwani makosa ya utakatishaji fedha hayana dhamana.
“Usiruhusu mtu apitishe fedha katika akaunti yako bila ufafanuzi wa kutosha, wote mtaingia katika kosa la utakatishaji fedha na mtakaa mahabusu hadi kesi imalizike,” alisema.
Kamanda Wekesi pia alitaka viongozi hao kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za kuchagua viongozi wa ngazi mbalimbali kwa misingi ya rushwa kwani hawatapata maendeleo.
Ofisa Uhamiaji mkoani Kilimanjaro, Martin Mwenda alitaka viongozi wa ngazi mbalimbali kuwa walinzi katika makazi yao kwa kutoruhusu kuwapo kwa wahamiaji haramu.