MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, amewataka wakuu wa wilaya za Maswa na Bariadi kuweka mikakati ya kudhibiti wanawake wanaojiuza kwa kuwa ni chanzo cha kusambaa kwa Virusi vya Ukimwi.
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, amewataka wakuu wa wilaya za Maswa na Bariadi kuweka mikakati ya kudhibiti wanawake wanaojiuza kwa kuwa ni chanzo cha kusambaa kwa Virusi vya Ukimwi. Aidha, alitaka kuchukuliwa hatua dhidi ya eneo la Malampaka maarufu DAR linalolalamikiwa na kinamama wa eneo hilo kwenye mikutano ya hadhara. Kafulila alitoa agizo hilo juzi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani iliyofanyika kimkoa wilayani Bariadi, ambaye alihamasisha wanaume kuacha tabia za kupima afya zao kwa kutumia majibu ya mke au mpenzi wake. Alisema kuwa amepata taarifa kuwa baadhi ya wadada wanajiuza maeneo mbalimbali na kuagiza wakuu wote wa wilaya kuhakikisha maeneo yote yanayotumika kwa biashara ya ngono yanadhibitiwa, kwani hiyo siyo biashara halali na utamaduni wa Watanzania. Aidha, aliziagiza kamati za amani na za usalama kukutana mara kwa mara na kuhakikisha zinashirikiana katika kudumisha maadili. "Serikali inaendelea kutumia rasimali watu,fedha na muda kuelimisha jamii kujikinga na Ukimwi, UVIKO16 na magonjwa mengine kwa sababu hakuna maendeleo yatapatikana kama taifa litapoteza nguvu kazi yake kwa vifo vinavyozuilika kwani ushindani wa dunia sasa upo kwenye ubora wa nguvu kazi ambayo inategemewa na kupimwa kwa vigezo hasa viwili, afya na maarifa," alisema. Kwa mujibu wa Kafulila, asilimia 43 ya maambukizi mapya Tanzania yanatokea kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24, hii ndio nguvu kazi ya nchi, na kwamba ni muhimu kuchukua hatua za haraka kwa kua huwezi kujenga taifa la vijana wenye afya dhaifu. "Pale utakapopima na kukutwa na VVU siyo mwisho wa maisha yako.Kupata haimaanishi ni mwisho wa maisha yako na mwisho wa kufanya kazi, hivyo tujitahidi kukabiliana na janga hilo.Tuwahi kupima ili tujue afya zetu,kwani kwa kuwahi kutumia dawa sahihi na kwa usahihi kutafubaza wadudu wa UKIMWI,” alisema Kafulila. Alisema takwimu zinaonyesha kuwa mkoani humo asilimia 84 ya wananchi wanatambua hali zao za maambukizi ya VVU.