Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ongezeko la fisi lawatisha wahifadhi, watafiti Ngorongoro

Sun, 25 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Wahifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyama (Tawiri) wameingiwa na hofu ya ongezeko kubwa la fisi katika eneo la Creta ya Ngorongoro ambao sasa wanamaliza watoto wa wanyama wengine.

Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk Fredy Manongi akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba 23, 2018 katika ziara ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constatine Kanyasu amesema katika eneo la kilometa za mraba 300 ndani ya Creta ya Ngorongoro kuna fisi 600 kwa sasa.

"Idadi hii ni kubwa sana kwani fisi hawa wamekuwa wakila watoto wa wanyama wengine na kusababisha wanyama kama chita kukimbia ndani ya Creta," amesema.

Amesema tayari kuna mradi wa fisi katika eneo hilo, umeanzishwa na hatua za kiuhifadhi zitachukuliwa ili kukabiliana na ongezeko hilo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk Simon Mduma amesema katika utafiti uliofanyika katika eneo la Ngorongoro, amebaini ongezeko kubwa la fisi ambao sasa ni tishio kwa wanyama na hata binadamu.

Dk Mduma amesema tayari tafiti zimeanza kubaini chanzo cha ongezeko hilo lakini pia kutafuta njia bora za kiuhifadhi kudhibiti ongezeko la fisi katika eneo hilo

Akizungumza baada ya taarifa ya wahifadhi na watafiti hao, Naibu Waziri Kanyasu ambaye yupo katika ziara ya kutembelea taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo, amewataka watafiti na wahifadhi kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.

Amesema kama fisi wakiongezeka sana, inawezekana isiwe tishio kwa wanyama pekee bali hata binadamu hasa watoto wanaoishi ndani ya mamlaka hiyo.

Katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro hadi sasa zaidi ya watoto wanne wa jamii ya Kimasai wameuawa na fisi baada ya fisi hao kuingia katika makazi yao.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kanyasu ameeleza kuridhishwa na ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuitaka mamlaka hiyo kuhamasisha wapangaji zaidi.



Chanzo: mwananchi.co.tz