Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ongezeko la bei ya maji lapingwa

18266 Maji+pic TanzaniaWeb

Thu, 20 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma/Ngara. Pendekezo la ongezeko la bei ya maji lililotangazwa na mamlaka za maji katika mikoa mbalimbali limeendelea kupingwa na wadau wakitaka zibakie kama zamani.

Akizungumza kwenye kikao cha wadau kuhusu maombi ya marekebisho ya bei za majisafi na majitaka kutoka Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira (Muwasa), Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema hakubaliani na kiwango cha upandishwaji wa bei hiyo iliyopendekezwa kutoka Sh850 hadi Sh2,310 kwa uniti.

Alisema anakataa kutokana na ukweli kwamba uniti moja ya maji ni sawa na ndoo kumi za maji hivyo hakuna sababu ya kupandisha bei ya maji kwa kuwa itakuwa ni kuwaumiza wananchi ambao hawana uwezo huo.

Meneja wa Muwasa, Robart Lupoja alisema bei mpya ya maji itakuwa Sh2,310 kutoka 850 ya awali kwa uniti.

Wakati huohuo; wadau na watumiaji maji katika halmashauri ya Ngara wamepinga ongezeko la bei ya maji kutoka Sh570 kwa wateja wa nyumbani na kufikia Sh1,450. Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura CCC), Hawa Ng’humbi kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam amepinga ombi hilo akidai Mamlaka ya Maji ya Mji wa Ngara haikufanya utafiti kujiridhisha kupata maoni ya wateja. Ng’humbi alisema kiwango kilichopendekezwa ni kikubwa kwa awamu ya kwanza na kinaumiza wananchi.

“Maoni ya wananchi yanaonyesha hasira na uchungu wa kukosa huduma ya maji ikiwa ni pamoja na kujinunulia mita licha ya kuwapo sababu au changamoto za uendeshaji na mapendekezo hayakuwa shirikishi katika mikutano ya watumiaji maji kwa kanda za huduma,” alisema Ng’humbi.

Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Ngara, Simon Ndyamukama alisema sababu za kupendekeza ongezeko la bei ni kutokana na uhaba wa fedha za uendeshaji na kuhitaji kuboresha miundombinu ya kusambaza maji.

Chanzo: mwananchi.co.tz