WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu Utumishi, kumuondoa kwenye nafasi yake Ofisa Manunuzi Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ili kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha za miradi.
Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo hayo mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo. Mchengerwa alisema uamuzi wa kumuondoa mtumishi huyo, unatokana na taarifa za kuwepo kwa mikataba mingi iliyosainiwa na baada ya muda ikafanyiwa mapitio na kuongezwa fedha jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
“Wakati uchunguzi unaendelea, Ofisa Manunuzi Mkuu huyo aripoti Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora siku ya Jumatatu (leo)na apelekwe Ofisa mwingine atakayetekeleza majukumu yake,” alisema Mchengerwa. Aidha, amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kupitia mikataba yote ya TARURA na kuchukua hatua stahiki pale itakapothibitika kuna ubadhirifu wa fedha.
“Namuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwenda TARURA kupitia mikataba yote kwa makini ili achukue hatua stahiki kwa watendaji ambao wanashiriki vitendo vya ubadhirifu vinavyokwamisha taifa kusonga mbele,” alisisitiza Mchengerwa. Mchengerwa alisema kama taifa, ni lazima kufanya maamuzi magumu pale inapobidi ili nchi iweze kupiga hatua katika maendeleo na wananchi wanufaike.
Alisema, Rais Samia Suluhu Hassan alipofungua fursa za kiuchumi katika utekelezaji wa miradi ya serikali, alitaka taifa lipige hatua katika maendeleo na sio watu wafanye ubadhirifu wa fedha za umma, hivyo tumuunge mkono kwa kupinga vitendo vinavyorudisha nyuma maendeleo.
Mchengerwa alisisitiza kuwa, Watumishi wa Umma hawana sababu ya kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ubadhirifu kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan anajali maslahi yao na yeye ni msikivu kwa watumishi. Mchengerwa alifanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Kagera ambapo amezungumza na watumishi, walengwa wa TASAF na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.