Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

OFISI ya Ardhi Mkoa wa Tabora imeanza mkakati wa kuyatambua maeneo yote ya wazi

B4d25eb57ac88a6c97e43cfb9935fa1a OFISI ya Ardhi Mkoa wa Tabora imeanza mkakati wa kuyatambua maeneo yote ya wazi

Mon, 19 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

OFISI ya Ardhi Mkoa wa Tabora imeanza mkakati wa kuyatambua maeneo yote ya wazi katika halmashauri za mkoa wa Tabora na kugawa ramani za maeneo hayo kwa watendaji wa kata ili kuyalinda maeneo hayo yasiweze kuvamiwa.

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki mkoani Tabora na Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora, Jabir Singano wakati akielezea utendaji kazi wa ofisi yake tangu kuzinduliwa rasmi mapema mwaka huu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikiwa ni mkakati wa serikali kusogeza huduma za sekta ya ardhi karibu na wananchi.

Alisema katika mkoa wa Tabora kumekuwa na tabia ya uvamizi wa maeneo ya wazi katika halmashauri za mkoa huo na katika kukabiliana na tatizo hilo ofisi yake imeanza mkakati wa kuyatembelea maeneo yote ya wazi katika halmashauri za mkoa huo na kuanza na Manispaa ya Tabora wakiwa na watendaji kata ili kuyatambua na kuwaonesha mipaka sambamba na kuwakabidhi ramani ili kuyalinda.

"Moja ya kitu nilichoelezwa na ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Tabora wakati ofisi yetu inaanza kazi ni suala la uvamizi maeneo ya wazi, hivyo tumeamua kulifanyia kazi kwa kuyatambua maeneo ya wazi na kugawa ramani za maeneo hayo kwa watendaji wa kata ili waweze kuyalinda na tumeanza na Manispaa ya Tabora na baadaye tutaendelea na halmashauri nyingine"alisema Singano.

Aidha Singano alisema mpango mwingine wa ofisi yake ya ardhi katika kuboresha sekta ya ardhi mkoani Tabora ni kukagua maeneo yote ya umma na kuanza na yale ya shule za msingi na sekondari kwa kubainisha mipaka, ambapo alisema lengo ni kuhakikisha maeneo yote ya umma hayavamiwi wakati ofisi ya ardhi mkoa ipo.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Mpera Manispaa ya Tabora, Grace Kasegezya aliishukuru ofisi ya ardhi mkoa wa Tabora kwa kuanza utambuzi maeneo ya wazi na kuwapatia ramani zinazoonesha maeneo ya wazi watendaji katika Kata za Manispaa ya Tabora.

Alisema kuoneshwa mipaka na kupatiwa ramani za maeneo ya wazi katika kata siyo tu kutawasaidia watendaji wa kata kutambua maeneo ya wazi bali kutawawezesha pia kama watendaji kuyafuatilia na kuyalinda dhidi ya uvamizi unaoweza kufanywa.

"Huu mpango unaofanywa na ofisi ya ardhi mkoa wa Tabora wa kutambua maeneo ya wazi na kutupatia ramani za maeneo hayo utatusaidia sana kuyatambua na kuyalinda hivyo niishukuru ofisi ya Kamishna wa Ardhi mkoa wa Tabora kwa kuanzisha hilo,”alisema Mtendaji Kata ya Mpera, Grace.

Chanzo: habarileo.co.tz