Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

OBC yadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh12 bilioni

51723 OBC+PIC

Thu, 11 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha imesema kati ya Januari na Machi mwaka huu, imebaini kampuni ya Otterlo Business Corporation Limited (OBC) kuisababishia Serikali hasara ya Sh12.483 bilioni.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoani Arusha, Frida Wikesi akizungumza na wanahabari ofisini kwake leo Alhamisi Aprili 11, 2019.

“Huyu (Isaya) Mollel amekuwa akiwahonga maofisa mbalimbali wa Serikali kwa lengo la kuwafanya  wawe watetezi wake katika mgogoro wa matumizi mseto wa Pori Tengefu la Loliondo huku akiwa ameisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha kwa kukwepa kulipa kodi,” amesema Wikesi.

Amesema Mollel na watuhumiwa wengine wamefikishwa mahakamani na taasisi hiyo na inaendelea na uchunguzi kuwabaini wahusika wengine  nao wafikishwe mahakamani.

Katika kipindi hichohicho Takukuru imepokea taarifa 138 kutoka sekta mbalimbali zikiwamo halmashauri (66), elimu (18), mahakama (13), polisi (12), ardhi (4), afya (4), kilimo (3), idara ya kazi (3), magereza (2) madini (2), maji  (2), Tanapa (2), NCAA (2), sekta ya utalii (1), Tanesco (1), Temdo (1), Mamlaka ya Mapato Tanzania (1) na Misitu (1).

“Taarifa hizi zimefunguliwa majalada 32 ya uchunguzi zipo katika hatua mbalimbali. Pia, ushauri umekuwa ukitolewa kwa watoa taarifa kwa malalamiko yanayoonekana kutokuangukia kwenye sheria yetu,” amesema Wikesi.

Pia, katika kipindi tajwa amesema Takukuru imefungua mashtaka mapya 11 mahakamani hadi sasa kesi 39 zinaendelea zikiwa katika hatua mbalimbali huku tayari ikiwa imeshinda matatu.

Wikesi ameongeza taasisi hiyo imeendelea kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika miradi miwili ambayo Serikali imewekeza Sh844.9 milioni ili kujiridhisha kama ina thamani ya fedha iliyotolewa.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni wa maji kijiji cha Malambo na ukarabati wa barabara za Wasso, Sakala, Loliondo, Olmesuit, Olorien, Magaiduru  hadi Mageri wilayani Ngorongoro.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz