Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nzige walioonekana Moshi wadaiwa kutoweka

95215 Pic+nzige Nzige walioonekana Moshi wadaiwa kutoweka

Tue, 11 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amesema kundi la nzige limeonekana jana Jumapili Februari 9, 2020 Wilaya ya Moshi na kisha kutokomea kusikojulikana, kwamba hadi leo Jumatatu Februari 10, 2020 hawajathibitisha walipo.

Ameeleza hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu taarifa za nzige hao kuingia Tanzania kutoka nchi jirani ya Kenya.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema juzi walipata taarifa kuwa nzige hao wapo kilometa 50 kufika Wilaya ya Mwanga lakini walifuatilia kwa watu wa Taveta nchini Kenya na kupata taarifa kuwa bado hawajafika, lakini jana jioni walionekana Wilaya ya Moshi na kupotea.

"Tulifuatilia Taveta lakini wao walituambia hawajafika kwao, hivyo tukajiridhisha hata kwetu hawajafika kwa kuwa hawajapita Taveta lakini jioni walionekana Moshi na kupotea" amesema.

Amebainisha kuwa kwa sasa wataalamu wako maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro ili kufanya ukaguzi na kujiridhisha kama kuna eneo ambalo nzige hao wameingia na taarifa itatolewa baada ya wataalamu hao kujiridhisha.

Amesema  kwa sasa vipepeo  ndiyo wameonekana wako wengi na tayari wamewasiliana na wataalamu nchini Kenya ambako pia wapo kwa wingi.

Pia Soma

Advertisement

Januari 29, 2020 Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Japhet Hasunga alisema Serikali itatumia ndege za kukodi kukabiliana na nzige ikiwa wataingia nchini kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda.

Ameeleza hayo mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tishio la nzige nchini.

Amesema walioonekana wilayani Loliondo walikuwa panzi si nzige.

Amebainisha kuwa Serikali imeandaa lita 7,000 za viuatilifu vya kuua nzige hao kwa kutumia ndege ambazo watazikodi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na shirika la kimataifa la kukabiliana na nzige.

Aliwataka wananchi na wadau wa kilimo kutoa taarifa ikiwa watabaini viashiria vya nzige katika maeneo yao.

Chanzo: mwananchi.co.tz