Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyumba 30 zilizoathiriwa na volcano ya matope kuhakikiwa

6ad40e81c2014e3683674b3b28da9978.jpeg Nyumba 30 zilizoathiriwa na volcano ya matope kuhakikiwa

Wed, 2 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KUTOKANA na changamoto ya volkano ya matope kuharibu nyumba kadhaa katika kata ya Kunduchi jijini Dar es Salaam, nyumba 30 zimeorodheshwa ili kufanyiwa uhakiki utakaochuja nyumba zinazopaswa kupatiwa fidia kabla ya kuvunjwa.

Akizungumza na HabariLEO jana, Mtendaji wa Kata ya Kunduchi, Ikunda Lyimo alisema kwa upande wa uongozi wa kata hiyo umeshakamilisha kuandikisha nyumba na kwasasa kinachosubiriwaa ni majibu kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa.

Alisema nyumba zilizoorodheshwa ni zile zilizokuwa karibu na eneo hilo lenye volkano na kwamba majibu ya ofisi ya mkuu wa mkoa ndiyo yatakayobainisha uhalali wa nyumba gani za kuvunjwa.

“Kata imekuwa karibu zaidi na wananchi hawa katika kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa, tumewatoa hofu na kuhakikisha kwa wale ambao hawana sababu ya kuhama kwa sasa waendelee kuwepo lakini nyumba moja wamehama tayari,” alisema.

Alisema nyumba ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKT) waliokuwa wakiishi ndani ya nyumba hiyo wamelazimika kuhama kwa kuwa walikuwa kwenye hatari zaidi.

“Kikubwa ambacho kwa sasa kinachoendelea ni kwa hao wakazi wenye nyumba hizo 30 kungojea majibu yao ya nani alipwe na nani asilipwe na wataambiwa nini cha kufanya,” alisema.

HabariLEO jsns lilifika kwenye eneo hilo lenye volkano ya matope na kukuta tangazo linalowatahadharisha wananchi na mifugo kupita huku likiwa limezungushiwa uzio.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na gazeti hili walionesha kustaajabishwa na hali hiyo huku wakisema kwa miaka waliyoishi katika eneo hilo hawajawahi kuona hali hiyo na tope kutoka ardhini likijaa juu ya ardhi.

Gazeti hili pia lilishuhudia nyumba moja ambayo imekatika nusu na kuzama huku nyingine zikionekana kuwa hatarini zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge alisema suala la wakazi hao linashughulikiwa na kwamba muda wowote tathmini hiyo itakamilika.

Tukio la volkano ya matope limeibua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakishangaa kuona tope zito likizidi kutoka na kujaa juu ya ardhi kisha kusambaa.

Wazazi hao wamekuwa na wasiwasi kuhusiana na usalama wao na watoto wao hasa wanafunzi ambao wamekuwa wakipita eneo hilo kwenda na kurudi shuleni.

Chanzo: habarileo.co.tz