Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyerere Square inavyogeuka kivutio kwa wageni Dodoma

Nyerere Square.png Nyerere Square inavyogeuka kivutio kwa wageni Dodoma

Mon, 15 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Eneo la Nyerere Square lililopo jijini Dodoma limekuwa kivutio cha watu wengi hasa wageni na mara nyingine wenyeji wake ambapo wamekuwa wakilitumia kama sehemu ya mapumziko hasa baada ya kazi ya kutwa nzima au mwishoni mwa juma.

Umaarufu wa eneo hilo unakuja kwa sababu watu wengi wanakuja kuangalia sanamu ya Rais wa awamu ya kwanza, hayati Mwalimu Julius Nyerere na kupiga nayo picha kama kumbukumbu zao.

Agnes Peter, mkazi wa Mbeya amekuja Dodoma kwa ajili ya shughuli zake binafsi, amezungumza na Mwananchi leo Aprili 14, 2024 na kueleza kwamba umaarufu wa eneo hilo siyo tu hapa Dodoma, bali hata huko mikoani na picha ya haraka inayowajia kichwani kuiona sanamu ya Mwalimu Nyerere.

“Nimekuja Dodoma kwa ajili ya Bunge Marathon lakini wakati tuko nyumbani tulikuwa tunasikia kuhusiana na eneo hili ambalo sanamu la Nyerere imesimikwa, kwa hiyo shauku yangu ilikuwa ni kujionea kwa macho yangu,” amesema Agnes.

Wenyeji wa mkoa huu wamesema licha ya kuwepo kwa maeneo mengine mapya ya kupumzikia, eneo hilo bado limekuwa bora kwa sababu ya kuboreshwa kwa baadhi ya vitu ikiwamo uwepo wa Intaneti ya bure ukiwa ndani ya eneo hilo.

Evarine Simon, mkazi wa Dodoma akizungumza na Mwananchi Digital kwenye eneo la Nyerere Square jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

Mkazi wa Dodoma, Everine Simon amesema kutotozwa gharama zozote za kuingia kwenye eneo hilo pia imekuwa sababu ya watu wengi kutembelea eneo hilo.

“Hapa pametulia sana, kwanza watu wameshapazoea, hata ikitokea serikali inapahamisha, watu watapata shida huko kwingine ni pembezoni kidogo mwa mji,” amesema Everine.

Kijana aliyejizolea umaarufu kwa talanta ya upigaji picha anayejulikana kwa jina la Don akiwawakilisha wafanyabiashara wanaotoa huduma ya picha, amesema sanamu ya Mwalimu Nyerere imekuwa na tija kwao kwani wateja wao wengi wamekuwa wakiwataka kupiga picha kwenye sanamu hiyo.

“Hii sanamu imebeba utambulisho wa mkoa wa Dodoma, hivyo wateja wetu wengi hasa wageni wamekuwa wakitaka kupiga nayo picha, kwa hiyo kwetu tunachukuwa kama faida,” amesema Don.

Picha ya sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo jijini Dodoma eneo la Nyerere Square.

Umaarufu wa Dodoma siyo zao la zabibu pekee, bali hata sanamu ya Mwalimu Nyerere ambayo inatajwa kubeba sura ya jiji la Dodoma na kuwafanya mamia ya watu wanaofika hapa kutaka kwenda kutembelea eneo la Nyerere Square.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live