WAKAZI wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wameshukuru kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Nyasa hadi Mbinga yenye urefu wa kilomita 66 inayojengwa na kampuni ya Chico ya nchini China.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema, kukamilika kwa barabara hiyo kunakwenda kumaliza changamoto ya mawasiliano kati ya wilaya hizo mbili na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa kwao.
Wamesema, uthubutu uliofanywa na serikali ya awamu ya tano kujenga barabara hiyo ni kati ya mambo mengi mazuri yaliyofanyika katika kipindi cha pili cha serikali ya awamu ya tano na sehemu ya kufungua fursa kiuchumi na ukuaji wa wilaya ya Nyasa ambapo Serikali imeweka alama ya kihistoria kwa vizazi vijavyo.
Wamesema, barabara hiyo ni kama zawadi kutoka kwa Serikali ya Rais John Magufuli kwa wananchi wa wilaya hiyo, ambao kwa muda mrefu walikuwa katika mateso makubwa kwa kukosa mawasiliano ya barabara ya uhakika.
Mbunge wa jimbo la Nyasa, Stella Manyanya alisema, kabla ya ujenzi wa barabara ya lami walikuwa wanatumia kati ya saa 12 hadi 16 kwenda Mbinga, lakini baada ya kukamilika kwa sasa wanatumia saa 1 hadi 1.30 kufika wilaya jirani ya Mbinga na masaa matatu kufika makao makuu ya mkoa Songea.
Wakati huo huo Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba, amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa kwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 103 na kuridhika na ujenzi wake.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo alisema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Nyasa na Watanzania kwa jumla.
Amesema, kukamilika kwa barabara kutasaidia sana wananchi wa Nyasa kusukuma maendeleo na kumaliza kero ya kusafiri muda mrefu kutoka Nyasa kwenda maeneo mengine ya mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kosmas Nshenye alisema, barabara hiyo ina manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwani wananchi wa Mbinga kwa sasa wana uhakika wa kusafirisha mazao yao kutoka shambani kwenda sokoni na kusafiri kwenda maeneo mengine kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Barabara ya Mbinga- Mbambabay yenye urefu wa kilomita 66, kilomita 50 ziko upande wa wilaya ya Mbinga .
Nayo kampuni ya Chico inayojenga barabara hiyo imesema ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa wakati kama ilivyoahidi kwa Rais John Magufuli wakati akiweka jiwe la msingi Aprili 2019.
Meneja msaidizi wa mradi huo Sam Han alisema, barabara hiyo kwa sasa imekamilika kwa asilimia 100.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Nyasa, Fidelix Duwe alisema, barabara hiyo ni ukombozi mkubwa kiuchumi na itafungua fursa mbalimbali kwa wananchi na fahari kubwa kuona ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa wakati sambamba na kuanza kwa safari za meli tatu katika ziwa Nyasa.
Kwa mujibu wake, barabara hiyo ina faida lukuki ikiwemo jamii ya wavuvi ambao watauza samaki moja kwa moja kutoka Nyasa kwenda katika masoko mbalimbali ya Mbinga na makao makuu ya mkoa mjini Songe.
Duwe ameipongeza kampuni ya Chico kutokana na uwezo mkubwa kujenga barabara kwa ubora wa hali ya juu na ameiomba Serikali kuhakikisha inashirikiana na kampuni ya Chico kwa kuipa kazi ya ujenzi wa miradi katika mikoa mbalimbali ambayo bado haijaunganishwa kwa barabara za lami.