Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyani wawatia hasira wananchi wakiharibu mazao shambani

Binadamu, Nyani Wanatumia Lugha Ya Ishara Inayofanana Nyani wawatia hasira wananchi wakiharibu mazao shambani

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi wa Kijiji cha Mnazibay, Kata ya Nalingu wamejikuta katika hali ngumu baada ya kushindwa kupanda mazao shambani kutokana na wingi nyani katika eneo hilo na kusababisha usumbufu kwao.

Akizungumza na Mwananchi Diwani wa Kata ya Nalingu Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Said Ally Amri amesema kuwa katika kijiji cha Mnazibay wameibuka nyani wengi ambao wameharibu mazao mbalimbali shambani.

“Yaani kwa sasa nyani ni changamoto kubwa wanyama wanaharibu mazao ya watu yaani wamekuwa na uharibifu mkubwa wa mzao ambapo wakifika wanakula hadi mabibo na kuondoka nayo yakiwa na korosho.

“Hii ndio miezi ya kupanda mazao na sasa tunaelekea kwenye kupanda ukienda kupanda bila kuchukua hatua tunaweza kushindwa kuvuna mazao hayo hivyo kuwepo kwa tatizo la chakula katika eneo hili,” amesema Amri.

Mohamed Ally Issa mkazi wa Mnazibay Nalingu amesema kuwa nyani wamekuwa shida kubwa yaani wamevamia mashamba yetu na sasa wanakuja majumbani.

“Kiuhalisia kijiji chetu kiko kando ya bahari maeneo yetu ukilima vyakula vinastawi na ukavuna kwa wingi lakini kwa nyani wametuvamia tumeshindwa kufanya lolote yaani kila unachopanda wanaharibu tumejaribu kila njia lakini hali si shwari tunaamini mamlaka zinazohusika zipo zinaweza kutusaidia,” amesema Issa.

“Yaani iwe mihogo, mbaazi, korosho na karanga wanakula kila kitu sasa tulipoacha kupanda ndio wanafata vyakula majumbani ukisahau mlango wazi wanaingia wanakula chakula,” amesema Issa.

"Tunaiomba serikali ifanye mpango itusaidei kuondoa hao nyani yaani wakiachwa wakazaliana zaidi nahisi tutahama kabisaa yaani wakikosa chakula shambani wanahamia majumbani yaani tuna wasiwasi kwakuwa tunaamini kuwa usalama wa watoto ni mdogo wanawaogopa,” amesema Issa

Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini Mashariki (Tawa), Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Abraham Jullu amesema kuwa Jeshi hilo litatuma askari wake waende kuangalia hali ilivyo na hatua gani wanaweza kuchukua.

“Yaani tumemaliza salama tatizo la tembo katika Wilaya ya Newala hali ni shwari kwa sasa, lakini kwenye nyani tunaenda kuangalia hali ikoje ndio tutatoa tathmini juu ya nini kifanyike,” amesema Kamanda Jullu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live