Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyani wageuka tishio kubwa Rombo

Nyani Pc Data Wanawake washindwa kwenda shamba wakihofia nyani

Tue, 9 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Baadhi ya wanawake katika vijiji vya Kata ya Kirongo Samanga wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, wanahofia kwenda mashambani kufanya shughuli zao za kilimo kwa madai ya kuvamiwa na makundi ya nyani.

Diwani wa kata hiyo, Prisila Shayo amesema nyani hao wamekuwa ni kero kubwa kwani imefika mahali hawaogopi wanawake.

"Hawa nyani wanatusumbua imefika mahali huku kwetu nyani hawaogopi wanawake wamekuwa ni wajanja kama binadamu, wakimwona mwanamke wanamvamia na kukudondosha chini kabisa," amesema diwani huyo.

Amesema wananchi ambao wameathiriwa zaidi ni wale walio pembezoni mwa bonde la Mlembea kutokana na wingi wa nyani waliopo katika eneo hilo, hali iliyowafanya washindwe kufanya shughuli za kilimo.

"Kipindi hiki watu ambao wamepakana na bonde la Mlembea wameshindwa kuotesha mahindi kabisa na mazao mengine kwa mfano zao kama la ndizi inawalazimu kuvalisha mfuko ili hawa nyani wasione maana huwa wanakula," amesema Prisila.

Baadhi ya wanawake waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wamesema kutokana na ongezo la nyani hao wameshindwa kujishughulisha na shughuli za kilimo.

Dementria Joseph ambaye ni mkazi wa kijiji cha Rima amesema kila mwaka mazao yao yanaliwa na nyani hao na kuambulia patupu hali ambayo imekuwa ni kikwazo kwa muda mrefu.

"Nyani wanatutesa sana kwa muda mrefu,tunashindwa kulima na hata kama umelima lazima uvalishe mazao yako suruali na shati ndio nyani waogope kuingia shambani lakini sisi wenyewe wanawake hawatuogopi, tunapigana nao vikumbo mashambani tuu,mwisho wa siku hakuna tunachovuna," amesema Dementria

Chanzo: mwananchidigital