Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyangwine atoa vitabu vya Sh10 milioni Shule ya Sekondari Dabalo

Mon, 15 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Chamwino. Mwandishi maarufu wa vitabu nchini, Nyambari Nyangwine ametoa vitabu vyenye thamani ya Sh10 milioni kwa Shule ya Sekondari Dabalo Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma huku akiahidi kutoa vitabu vyenye thamani ya Sh22 milioni kwa Jimbo la Chilonwa wilayani hapa.

Akizungumza katika mahafali ya 16 ya shule hiyo, Nyangwine amesema kwa kutambua jitihada za Serikali za utoaji wa elimu bure nchini ameamua kutoa vitabu hivyo ikiwa ni mchango wake katika sekta ya elimu.

Amesema vitabu hivyo alivyovitoa kwa shule ya sekondari Dabalo ni vya masomo yote na vitawasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani iliyopo mbele yao.

“Kwa siku chache zilizobaki ili kidato cha nne mfanye mitihani mnaweza kuvitumia vitabu hivi na mkafaulu vizuri mitihani yenu, niwaahidi kuwa kila mwanafunzi atakayefaulu kujiunga na kidato cha tano nitamnunulia vitabu vyote vya masomo yote ya ‘A level’ hivyo hakikisheni mnafanya vizuri katika mitihani yenu,” amesema Nyangwine.

Hata hivyo, ameahidi kutoa kompyuta mbili na mashine ya kutolea nakala ili kuwasaidia walimu kuweza kuchapisha mitihani ya mara kwa mara badala ya kuandika ubaoni.

Akizungumzia vitabu hivyo vyenye thamani ya Sh22 milioni Nyangwine amesema vitabu vya Sh2 milioni ni vya shule za msingi, Kata ya Dabalo na vitu vya Sh20 milioni ni kwa ajili ya shule zilizopo katika Jimbo la Chilonwa.

“Vitabu hivyo vya shule ya msingi nitamkabidhi Diwani wa Dabalo (Elisha Matewa) na hivyo vya shule za Jimbo la Chilonwa nitamkabidhi mbunge wenu (Joel Mwaka), vitabu hivyo nitavitoa ndani ya muda mfupi kuanzia sasa,” amesema.

Nyangwine aliyewahi kuwa mbunge wa Tarime (CCM) mkoani Mara ametumia nafasi hiyo kuwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kutatua changamoto zilizopo hasa ya ujinga kupitia elimu waliyonayo.

 

Awali, akizungumza katika mahafali hayo mkuu wa shule ya sekondari Dabalo, Vicent Kantaule amesema changamoto zinazoikabili shule hiyo ni uhaba wa vitabu, kompyuta, mashine ya kutolea nakala na ukumbi wa shule.

Amesema shule ina wanafunzi 239 na walimu 15 wa masomo mbalimbali lakini somo la fizikia halina mwalimu.

“Tunaomba tusaidiwe kupata walimu wa somo la Fizikia kwani somo hili hatuna mwalimu wa kulifundisha. Pamoja na changamoto hizo shule yetu imejenga hosteli mbili moja ya wasichana na moja ya wavulana lengo ni kuhakikisha tunajenga majengo mengine ili wanafunzi wote wakae hosteli,” amesema  Kantaule.

Mbunge wa jimbo hilo, Mwaka amemshukuru Nyangwine kwa mchango wake katika sekta ya elimu kwenye jimbo hilo huku akisema vitabu hivyo vitasaidia kuinua kiwango cha elimu kwa shule za msingi na sekondari.

Chanzo: mwananchi.co.tz