Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Njoolay akumbuka alivyomhoji Mkapa kumteua RC

034651a37ad9d2b690f6e413e19076d1 Njoolay akumbuka alivyomhoji Mkapa kumteua RC

Tue, 28 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ALIYEWAHI kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daniel ole Njoolay amesema alipoteuliwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa alishtuka lakini alimuuliza kwa nini amemteua.

Aidha amesema wakati wa uhai wake, Mkapa alipenda kuambiwa ukweli hata kama mchungu kwake.

Njoolay alisema hayo jana jijini Dares Salaam katika uwanja wa Uhuru ambapo alishiriki katika tukio la kuaga mwili wa kiongozi huyo.

“Aliponiteua kwenye nafasi ya ukuu wa mkoa nilishtuka sana, siku ile anaapisha nilimuuliza kwa nini umeniteua wakati sijawahi kufanya kazi serikalini?,” alisema Njoolay bila kueleza majibu aliyopewa na Mkapa.

Kuhusu aliyoyafanya akiwa kwenye nafasi hiyo katika uongozi wa Rais Mkapa alisema alimshauri Mkapa kugawa mkoa wa Arusha na Manyara na alisimamia ujenzi wa shule nyingi za sekondari jambo lililomfurahisha Mkapa.

Alisema pia aliweza kuboresha mazingira kwa kupanda miti mingi mkoani humo na baadaye Rais Mkapa alimhamishia Mkoa wa Mwanza ambao nao aliuboresha na kujenga shule za kata. Mkapa alipofika mkoani humo alishangaa idadi ya shule zilizojengwa kwa nguvu za wananchi.

Aidha alisema aliboresha na kuipanua Hospitali ya Sekou Toure kwa nguvu za wananchi ambapo alifurahi na alizidi kumwamini zaidi.

Njoolay alisema Rais Mkapa alipenda kuambiwa ukweli hata kama ni mchungu na kwamba aliweza kumshauri kutohitimisha kampeni eneo la Karatu kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na kwamba Chama cha Mapinduzi(CCM) hakijashinda na alikubali.

“Nilimwambia kule Karatu si vizuri kuhitimisha kampeni bado hatujashinda, lakini yeye (Mkapa) alihoji mbona kuanzia kule uwanja wa ndege wanasema lazima tushinde?,” alisema.

Njoolay aliongeza kuwa siku ya uchaguzi kule Karatu walianguka na siku ya sherehe Ikulu Mkapa aliwachekesha kuna waganga wa kienyeji wanaoweza kutabiri akirejea Karatu.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka alimzungumzia Rais mstaafu Mkapa kama kiongozi madhubuti na makini asiyeyumbishwa.

Alisema alitimiza wajibu wake ipasavyo na aliweza kuieleza dunia maamuzi ya nchi kupeleka jeshi Uganda kupigana na Idd Amin kutokana na kusikiliza vyema misimamo ya Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere.

Alisema alikuwa na uwezo mkubwa kujieleza na kutokana na kumfahamu kwa karibu alijua alikuwa na misimamo na alikiri alikabidhiwa nchi ikiwa salama na angeiacha salama.

Kuhusu uongozi wake kwenye CCM, alisema aliamini katika misingi ya katiba na kanuni za chama, akiweka mbele maslahi ya nchi, kufuata utaratibu na kuamini wagombea wenye sifa.

Chanzo: habarileo.co.tz