Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Njoolay, Shirima waeleza siri Mkapa Mkurabita

D87542f2a7ce4587a33d146587ebebbf Njoolay, Shirima waeleza siri Mkapa Mkurabita

Thu, 30 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa alianzisha Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) kuwatoa Watanzania katika unyonge na umaskini.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mkurabita, Balozi Daniel ole Njoolay na Mkuu wa Mkoa Mstaafu wa Mtwara na Arusha, Isidori Shirima wakimzungumzia Hayati Mkapa.

Walikuwa wakizungumza katika hafla taasisi hiyo kugawa hatimiliki za kimila 465 za ardhi kwa wanavijiji wa Jaribu-Mpakani, Nyamisati, Kivinja B na Mchukwi A katika Kata ya Mjawa wilayani Kibiti katika Mkoa wa Pwani.

Hati hizo ziligawiwa baada ya wananchi hao kupimiwa mashamba, kuhakikiwa, kuandaliwa hati hizo kwa kuwezeshwa na Mkurabita. Katika hafla hiyo kijijini Jaribu- Mpakani, Njoolay, Shirima na Mratibu wa Kitaifa wa Mkurabita, Dk Seraphia Mgembe walisema Mkapa alianzisha Mkurabita mwaka 2004.

Walisema aliianzisha ili kufanya rasilimali za wanyonge zitambulike kisheria katika vyombo vya fedha na kutumika kukuza mitaji yao.

“Mkapa alilenga kufanya rasilimali na biashara za wanyonge kuwa rasmi na zenye tija, hivyo zitumieni vizuri hati ziwasaidie kuondokana na umaskini kwa kupata pesa na kuzitumia vizuri kukuza mitaji, kula vizuri, nyumba nzuri na kusomesha watoto…” alisema Njoolay.

Alisema taarifa zinaonesha wananchi waliopata hati hizo na kuzitumia vizuri, wamekopa zaidi ya Sh bilioni 25 katika benki mbalimbali nchini. Alisema Mkurabita watatoa mafunzo ya kutumia hati hizo kupata na kukuza mitaji.

Naye Shirima alisema: “Mkurabita ni matunda ya utekelezaji wa sera aliyoasisi Mzee Mkapa ili wanyonge watumie mitaji yao ikiwamo ardhi kushiriki, kumiliki na kujiinua kiuchumi.”

Kwa upande wake, Dk Mgembe alisema: “Mkurabita tutafanya kazi usiku na mchana kuhakisha ndoto ya Mzee Mkapa kuwafanya wanyonge waondokane na umaskini inatimia.”

Dk Mgembe alihimiza waliopata hatimiliki hizo za kimila za ardhi kuepuka tamaa ya kuuza mashamba yao ili waendelee kunufaika. “Niwaombe msiuze mashamba yenu kiholela; mtajuta baadaye… ardhi yenu ni nzuri na mko karibu na Dar es Salaam, eneo la kiuchumi; najua wengi watakuja kuwashawishi muwauzie; msikubali mtajuta,” alisema Dk Mgembe.

Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, mkoa wa Pwani, Mohamed Mavura, alisema; “Kibiti tuna vijiji Kata 16 na vijiji 58 hivyo, tuna kazi kubwa kuhakikisha vijiji vyote vinanufaika na Mkurabita…” Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibiti, Milongo Sanga aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya katika hafla hiyo, alionya dhidi ya kasumba ya baadhi ya watu kupata pesa na kuzifuja kwa kufanyia sherehe huku wanaume wakioa wake zaidi.

Alisema mwaka 2009 hadi 2010 mashamba 1,600 yalipimwa Kibiti, lakini zimetoka hati 465 kwani wakati wa uhakiki yalibainika mashamba mengi yenye migogoro, wamiliki kufariki dunia na taratibu zake za mirathi kutokamilika. Pia alisema, baadhi ya wananchi walipuuza na kutojitokeza kuhakiki taarifa zao na mashamba mengine kupitiwa na mradi wa bomba la gesi.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Jaribu-Mpakani, Shamte Cheke, alisema kijijini kwake, taarifa zilizopatikana ni 884, waliopata hati ni 327.

“Wanakijiji 388 hawakujitokeza kuhakiki, 85 walifariki dunia, watano hawajulikani walipo, yaliyouzwa ni 68 na mradi wa Songas ulipitia 11.”

Chanzo: habarileo.co.tz