Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nishati jadidifu ilivyobadili maisha kijiji cha Lukumbule

60552 Lukumbule+pc

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kama mara yako ya mwisho kufika Kijjji cha Lukumbule wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma ni mwaka 2017, huwezi kuamini macho yako ukifika sasa kutokana na maendeleo ya shughuli za kiuchumi.

Lukumbule inapatikana Kusini mwa Tunduru umbali wa kilomita 64 kutoka Tunduru mjini hadi katika kijiji hicho kilichopo Kata na Tarafa ya Lukumbule.

Unapoanza kuingia katika kijiji hicho utaanza kukaribishwa na nguzo na nyaya za umeme ambazo ndizo zimeleta neema kwa wakazi wa kijiji hicho. Kutokana na uwepo wa umeme wa uhakika wananchi wameanzisha shughuli mbalimbali ikiwamo viwanda vidogovidogo vya uchomeleaji, maduka yenye majokofu, saluni za kunyoa nywele na kupamba.

Ujio wa nishati jadidifu ya umeme jua katika kijiji hicho umepeleka mwanga mpya kwa maisha ya wananchi ambao wanautumia kwa shughuli mbalimbali ikiwamo matumizi ya majumbani, pia wamewekeza katika miradi ya kiuchumi.

Mmoja wa wanufaika wa nishati hiyo inayozalishwa na kusambazwa na kampuni ya PowerCorner, Malidadi Abina ambaye ni fundi wa kuchomelea anasema licha ya kupanua shughuli zake na kuongeza kipato, pia ametengeneza fursa ya ajira kwa vijana wawili wanaomsaidia kazi zake.

“Kupitia matumizi ya umeme, sasa naingiza zaidi ya Sh95,000 kwa wiki tofauti na Sh20,000 nilizokuwa nikiingiza kabla ya ujio wa umeme,” anasema Abina.

Pia Soma

Hadija Issa ambaye watoto wake sasa wanapata urahisi wa kujisomea usiku tofauti na awali walipokuwa wakitegemea taa za vibatari na chemli anasema umeme huo ni mkombozi.

Hadija anasema uwepo wa nishati jadidifu umewafungulia milango ya kutazama runinga kufahamu kinachojiri nchini na nje ya nchi.

“Familia yangu pia hupata fursa ya kuangalia vipindi vya runinga ikiwamo tamthilia na taarifa za habari,” anasema Hadija.

Juma Ayubu yeye baada ya ujio wa nishati jadidifu, anasema ameondokana na kero ya kusafiri kilomita 64 hadi mjini Tunduru kupata huduma za ‘steshenari’ kama kuchapa na kurudufu nyaraka.

Msimamizi wa mradi wa PowerCorner katika kijiji hicho, Adam Issa anasema kwa sasa wana wateja 150 na lengo ni kufikia 400 hadi 600.

“Lengo ni kufikia wateja 400, lakini kutokana na wananchi kuonyesha nia ya uhitaji tunaweza kufikia wateja 600 kutoka 150 ambao tunao sasa na tayari tunayo maombi ya wateja wasiopungua 50. Siku zinavyozidi kwenda wanazidi kuelewa nishati jadidifu na kuupokea mradi,” anasema.

Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Lukumbule, Bahati Andrea, anasema kaya 140 kati ya 198 zenye wakazi 5,427 katika kijiji hicho tayari zimejiunga au kuomba kuunganishiwa umeme huo.

Mtaalamu nishati jadidifu

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Kiuchumi kwa Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas), Mahama Kappiah anataja nishati jadidifu kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya kutiliwa maanani na yanayokopesheka.

Akizungumza wakati wa mkutano wa wiki ya hali ya hewa Afrika iliyofanyika Machi mwaka huu jijini Accra, Ghana, Kappiah anazitaka nchi za Afrika kuwekeza kwenye nishati jadidifu kwani miradi hiyo inakubalika na kukopesheka kwenye taasisi za kifedha za kimataifa ikiwamo Benki ya Dunia.

“Zaidi ya watu 1.3 bilioni duniani kati yao 700 milioni wakiwa barani Afrika wanatarajia kuunganishwa na nishati jadidifu ambayo ni rafiki kwa watumiaji na mazingira,” anasema.

Meneja mradi huo, Daniel Nickson anasema gharama za mteja kuunganishiwa huduma ni kati ya Sh29,000 hadi Sh177,000 kulingana na mahitaji ya mtumiaji, huku vifaa vyote kama nguzo na ‘bulbu’ zikitolewa na kampuni hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz