Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametaja kilichosababisha mikoa ya Lindi na Mtwara kuchelewa kupata maendeleo.
Akihutubia wananchi wa Jimbo la Rwangwa mkoani Lindi leo Jumanne Oktoba 15, 2019, Rais Magufuli amesema anafahamu changamoto nyingi za barabara zinazoikabili mikoa hiyo.
Amesema baada ya Tanzania kupata uhuru, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliamua mikoa hiyo itumike kwa ajili ya ukombozi wa nchi nyingine za kusini mwa Afrika.
“Ninafahamu changamoto ya barabara nyingi katika maeneo ya mkoa wa Lindi na Mtwara, napenda nikiri tangu tupate uhuru hatukuitendea haki sana mikoa hii miwili, kukiri ni kitu kizuri, kukiri ni heshima, kukiri ni uungwana,” amesema Rais Magufuli na kuongeza;
“Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara mnafahamu ninyi wenyewe sababu zipi za msingi zilizofanya kutoendelea na kuwa na miundombinu duni.”
Amesema mikoa hiyo ilitumika kuwapa mafunzo wapigania uhuru jambo lililosababisha kuchelewa kujengwa barabara kwa sababu za kiusalama.
Pia Soma
- Akina mama wazuriwazuri wamchelewesha Rais Magufuli
- Mwonekano wa Wilaya ya Rungwa ya miaka ile si wa sasa- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
- Magufuli aahidi kuwalipa wakulima wa Korosho jimboni kwa Nape
Amesema wakati huu ni zamu ya kufufua maendeleo katika mikoa hiyo huku akiahidi kujenga barabara zilizoombwa na wabunge wa mkoa huo.
“Waheshimiwa wabunge naomba mniachie, nimewasikia,” amesema kiongozi huyo wa nchi.
Amewataka wananchi wa Jimbo la Rwanga kuendelea kutoa ushirikiano kwa mbunge wao, Kassim Majaliwa, madiwani na Serikali kwa ujumla.
“Mlinichagua bure ni lazima nitumike bure, ndiyo maana namuomba sana Mwenyezi Mungu nisije nikawa na kiburi,” amesema Rais Magufuli.