Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngubiagai: Tumieni mikopo kwa malengo

1ca5d196208ed9f0643a80b8b1cc1bfd Ngubiagai: Tumieni mikopo kwa malengo

Fri, 13 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai amewataka wananchi wanaopokea mikopo kutoka katika halmashauri hiyo kwa mujibu wa sheria kutotumia mikopo hiyo kinyume na maombi yao.

Alisema hayo wakati akikabidhi hundi ya Sh milioni 168.5 kwa vikundi 43 vya wilaya hiyo, mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kama inavyotakiwa kisheria.

Katika makabidhiano hayo ambapo watendaji mbalimbali wa serikali walikuwepo wakiwawemo Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji, Gloria Mbasha na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa, Ayoub Kiponza, Ngubiagai alisema ni kosa na hatari kutumia mkopo kinyume na malengo yaliyokusudiwa.

Alisema fedha hizo ni matokeo ya mipango safi ya Serikali ya Awamu ya Tano yenye lengo la kuwapatia mitaji wanawake, vijana na walemavu ili waboreshe maisha yao na kuinua kipato cha familia, wilaya, mkoa na taifa kwa jumla.

Alisema fedha hizo zikitumiwa kwa mujibu wa maandiko ya mradi, ni dhahiri zitasaidia kutatengeneza ajira sahihi na kuongeza pato la makundi hayo.

Aliwataka waliopatiwa fedha hizo kuhakikisha wanarejesha ili kuwezesha wengine nao kukopa, hivyo kuwa na uhakika wa kuinua makundi mengi kiuchumi kwa kuzingatia taratibu zilizopo.

Aidha, aliwataka wajasiriamali hao kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kuzingatia ubunifu kama sehemu muhimu ya kuendeleza ujasiriamali wao kufikia hatua za juu zaidi.

Mkuu wa Wilaya huyo alisema ni vyema waliochukua fedha hizo kuhakikisha kwamba malengo yanafikiwa kwa kupenda wanachokifanya na kukithamini huku wakijifunza kuwa na uvumilivu.

Alishukuru mashirika ya Action Aid na Tanganyika Christian Refugees Services (TCRS) kwa kuwafunza wajasiriamali ili wajitambue na kupiga kasi katika maendeleo ya makundi hayo maalumu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kilwa, Godfrey Jafari, aliwaonya waliochukua mikopo na hawajarejesha kutambua kwamba, vitendo vyao vinazuia maendeleo yao na ya wenzao.

Jafari aliwataka waliochukua mikopo kutambua kuwa, wasipoitumia ipasavyo, wanaweza kuibua hisia tofauti kwa jamii na wao wenyewe kushindwa kuendelea.

Baadhi ya wanufaika mikopo hiyo Zahan Ahmad na Nuru Magoma wa Kijiji cha Likawale walishukuru serikali kwa kutambua mahitaji yao na kuahidi kufanyakazi kwa bidiii kuhakikisha ili kurejesha kwa wakati na kuomba zaidi.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Kilwa, Grace Mwambe, alisema halmashauri hiyo imefanya vyema kuhakikisha makundi ya vijana, wanawake na walemavu yanapata mitaji ya kuanzia shughuli zao.

Aidha, aliwataka walemavu kujiunga katika makundi na kufaidi mitaji inayofanyiwa kazi na halmshauri.

Chanzo: habarileo.co.tz