Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngara walia vitambulisho vya NIDA

NIDA JULAI Ngara walia vitambulisho vya NIDA

Fri, 28 Jul 2023 Chanzo: mwanachidigital

Kilio cha kukosa namba na Vitambulisho vya Taifa (Nida) na kuporomoka kwa bei ya kahawa ni miongoni mwa changamoto za wananchi zinazotawala mikutano ya hadhara ya Mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoro inayoendelea katika vijiji tofauti.

Wakati hoja kuhusu namba na vitambulisho vya NIDA zimetawala katika mikutano iliyofanyika katika kata zinazopakana na nchi jirani za Rwanda na Burundi, suala la kuporomoka kwa bei ya kahawa kutoka zaidi ya Sh3, 000 hadi kufikia Sh1, 900 zimetolewa na wakulima wa zao hilo wilayani Ngara.

‘’Nimetumia gharama mara kadhaa kwa kukodisha pikipiki kwa Sh10, 000 kwenda na kurudi ofisi za NIDA mjini Ngara kutafuta ama namba au kitambulisho bila mafanikio. Tunaiomba Serikali ituondolee kero hii kwa kuhakikisha wote wenye sifa tunapata namba au vitambulisho,’’ amekaririwa Heziron Bisekwa, mkazi wa kijiji cha Kigina Kata ya Ntobeye inayopakana nan chi jirani ya Burundi

Katika maelezo yake yaliyoonekana kuungwa mkono kwa kupigiwa makofi na wananchi uliohudhuria mkutano huo, Bisekwa amesema kukosa namba na vitambulisho kunawanyima wananchi huduma za siyo tu za Kiserikali, bali pia za kifedha na usajili wa laini za simu.

Hidaya Athman, mkazi mwingine wa Kijiji cha Kigina amesema kukosa namba na vitambulisho vya NIDA ni tatizo sugu lisilopatiwa ufumbzi licha ya ahadi kadhaa zinazotolewa na wagombea wa vyama mbalimbali nyakati za kampeni za uchaguzi.

Diwani wa Kata ya Ntobeya, Sande Mkozi ameunga mkono malalamiko ya wananchi akisema jitihada zake na viongozi wengine za kutafutia ufumbuzi tatizo hilo hazijazaa matundo na kumwomba mbunge Ruhoro kusaidia suala hilo.

‘’Kata ya Ntobeya ina zaidi ya watu 25,000 wenye sifa ya kupata vitambulisho vya Taifa; lakini ni watu wasiozidi 500 ndio wamefanikiwa kupata vitambulishi huko wengine wanaokadiriwa kufikia 2, 000 wakiwa na namba. Hii ni kero inayotunyima usingizi viongozi,’’ amesema diwani Mkozi

Akizungumzia kushuka kwa bei ya ya kahawa aina ya Arabika kutoka Sh3, 020 hadi Sh1, 900, Ramadhani Abdul, mkulima wa kahawa kutoka kijiji cha Kigina amesema licha ya jitihada za Chama cha Ushirika Ngara (Ngara Farmers’ cooperative Society) za kutafuta bei nzuri, bado bei ya zao hilo inazidi kuporomoka.

Akijibu hoja ya namba na vitambulisho vya NIDA, Mbunge Ruhoro ameahidi kufuatilia suala hilo huku akiwatupia lawama wananchi kwa kukwepa kujitokeza kuhakiki taarifa zao kwa takribani mara mbili wakati maofisa wa NIDA walipofika kwenye maeneo yao.

“Mwaka 2020 niliahidi kuwaleta maofisa wa NIDA na uhamiaji katika kata za mpakani zenye changamoto ya namba na vitambulisjo na nilitimiza ahadi hiyo kwa kuwaleta maofisa hao hapa Kata ya Ntobeye na mwaka mwaka 2021. Mwaka 2022 pia walirejea lakini wananchi hawakujitokeza kuhakikiwa taarifa zao. Hii inakatisha tamaa,’’ amesema mbunge Ruhoro

Mbunge huyo ameahidi kuwapeleka tena maofisa wa NIDA na Uhamiaji katika kata hiyo mwaka 2024 na kuwasihi wananchi kujitokeza kuhakiki taarifa zao ili kumaliza kero ya kukosa namba na vitambulisho vya Taifa.

Kuhusu bei ya kahawa, mbunge Ruhoro amewashauri wakulima kuuza mazao yao mapema kuepuka madhara ya bei kushuka zaidi kutokana na changamoto za kiuchumi zinazoikumba soko la dunia zinazochangiwa na mambo kadhaa ikiwemo vita vya Urusi na Ukraine.

Chanzo: mwanachidigital