Ng'ombe 547 wamekamatwa wakichungwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kinyume cha sheria, huku wachungaji wakikimbia na kuitelekeza mifugo hiyo.
Hifadhi hiyo ni kati ya maeneo ambayo yamekuwa yakiharibiwa na kusababisha madhara ya kimazingira, ikiwemo kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu.
Akizungumzia suala hilo leo Jumatano Machi 27, 2024, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Godwell Meng'ataki amesema ilikamatwa eneo la Ukwaheri ndani ya bonde lenye ardhi oevu la Usangu.
Amesema wamekuwa wakiendelea kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira, hususani katika bonde hilo lenye vyanzo muhimu vya maji kwa ajili ya mto Ruaha Mkuu na bioanuai muhimu kwa mazingira, uhifadhi na utalii.
Amesema Mahakama imeshatoa amri mifugo hiyo itaifishwe na imeshateua dalali wa kuiuza.
“Kuna kazi kubwa imefanywa na vikosi vyetu vya askari wakishirikiana na vingine vya doria, ambao walibaini uwepo wa ng'ombe ndani ya eneo la Ihefu na wamewakamata 547 na punda watatu. Mifugo hii imekuwa ikifanya uharibifu ndani ya hifadhi, tumekuwa tunafanya kazi kubwa ya kulinda bonde hili.”
“Hivi karibuni walibadili utaratibu wakawa wanaiingiza usiku na kuiondoa usiku, lakini tunaporuka na ndege katika maeneo haya tunabaini uwepo wa mifugo pembezoni mwa hifadhi," amesema na kuongeza;
"Nitoe wito waliozoea tabia hiyo waiache, vinginevyo wataendelea kupoteza mifugo yao kwa sababu tutapeleka kwenye vyombo vya sheria na hakuna aliye juu ya sheria, kwa hiyo ni vema wakachukua hatua ya kuepuka kuingiza mifugo hifadhini.
Amesema, “tukumbuke kupitia mito ambayo inaingiza maji katika bonde hili ndipo tunapata chanzo katika Mto Ruaha Mkuu ambao ni muhimu katika nchi yetu, unatumika kuzalisha umeme katika mabwawa ya Mtera, Kidatu na Bwawa la Julius Nyerere.
Ameeleza jitihada za uhifadhi katika bonde hilo zitaendelea kwa nguvu zote, ikiwemo kupitia doria za miguu, anga, magari na kushirikiana na wananchi wanaozunguka eneo hilo.
Mkuu wa Kanda ya Usangu, Mhifadhi daraja la pili Abisai Nassari, ametaja baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ni maeneo ambayo mifugo inawekwa ikishaingizwa katika hifadhi kuwa magumu kufikika.
Amesema mifugo huingizwa katikati ya matindiga, inakuwa vigumu kwa askari kufika hivyo kulazimika kushirikiana na kikosi cha anga kuyafikia na kusogeza mifugo kwenye maeneo mengine ambayo askari wanaweza kufika.
"Pia tunakabiliana na changamoto ya uvamizi, baada ya kuichukua mifugo, wanajipanga kwa kutumia mbinu zao wanakuja na mishale na wanajaribu kutuvamia ila tunakabiliana nao,” amesema.
Amesema mifugo hupelekwa maeneo ambayo hakuna mawasiliano, hivyo ni vigumu ukiwa eneo la tukio kupata msaada, wanajipanga kuwa na vikosi vya aina tofauti.