Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Neno la mwisho la Mtega kwa familia yake

Mtega 688456106016 Neno la mwisho la Mtega kwa familia yake

Tue, 4 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

"Aliniambia nisimamie mali na kazi kwa umakini mkubwa." Hiyo ni kauli ya Adolf Francis, mtoto wa kwanza wa aliyekuwa mbunge wa Mbarali, Francis Mtega anayesema baba yake alitoa kauli hiyo kwa mara ya mwisho Jumamosi Julai mosi, kabla ya kuanza safari kuelekea shambani.

Mtega alipatwa na mauti wakati akirejea kutoka shambani kwake kwa kugongwa na trekta dogo 'Power Tilla' saa 9 alasiri.

Mwili wa mbunge huyo utaagwa kesho jimboni humo kabla ya kusafirishwa kwenda wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe kwa maziko yatakayofanyika Jumatano.

Akizungumza na Mwananchi jana nyumbani kwa marehemu katika Kitongoji cha Tazara, Kijiji cha Lyambogo, wilayani Mbarari, Adolf alisema ni pigo kwao kumpoteza mzazi aliyekuwa msaada mkubwa kwa familia na sasa limebaki pengo ambalo katu halizibiki.

Huku akitokwa na machozi, alisema siku hiyo pia baba yake alimtaka akaangalie mifugo iliyokuwa imevamia shambani. “Nilienda shambani tukakuta kuna uharibifu mkubwa uliofanywa, nikampigia simu kumwelezea, nakumbuka alichonisisitiza ni kusimamia kwa umakini kazi na mali. Hilo ndio nalikumbuka kwa haraka, hakika ni pigo na pengo kubwa kwetu,” amesema. Adolf amesema baba yake amewaacha watoto wanne, watatu wakubwa wanajitegemea na mmoja mdogo ambayekwa sasa yuko kidato cha tano.

Hali ilivyo nyumbani

Jana, nyumbani kwa Mtega vilio, simanzi na huzuni viliendelea kutawala huku viongozi mbalimbali wakiwamo wa vyama vya siasa na Serikali walifika kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Akizungumzia msiba huo, mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbarali, Mathayo Mwangomo amesema imekuwa pigo kubwa kwa jamii na chama kwa ujumla kuondokewa na kiongozi huyo aliyekuwa mpenda watu na maendeleo.

Amesema katika uhai wake alipenda kuwaunganisha wananchi, kushirikiana na jamii kwenye miradi ya maendeleo na kwamba kabla ya kuombwa na wananchi kugombea ubunge aliwahi kuwa diwani na mwenyekiti wa Halmashauri Mbarali.

“Jumanne itakuwa siku ya kuaga mwili na kutoa salamu za rambirambi hapa nyumbani kwake, kisha Jumatano mwili utasafirishwa kuelekea nyumbani kwao Ludewa Njombe kwa taratibu za mazishi. “Tutamkumbuka kwa mengi mbunge wetu na moja ya ahadi zake ilikuwa kuunganisha wananchi kitu ambacho alifanikiwa, pia alichangia na kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo " alisema Mwangomo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Msalaka, Lufunyo Mwafute alisema miongoni mwa ahadi ambazo mbunge huyo aliahidi enzi za uhai wake ambazo zilikuwa hazijakamilika ni mradi mkubwa wa maji na Shule ya Sekondari Mwale ambayo ilikuwa haijaisha.

“Amefanya mambo mengi makubwa ikiwamo kituo cha afya na mengine tuna wasiwasi kama yataisha haraka kama mradi wa maji na ujenzi wa bweni kwenye Shule ya Sekondari Mwale. Pia alisaidia ujenzi wa Shule ya Msingi Lyambogo na skimu ya maji Igumbilo," amesema na kuongeza:

"Alikuwa msaada mkubwa kwetu hakubagua mzee, kijana wala mtu yeyote. Alikuwa akisaidia hata mtu mmoja mmoja, hivyo ni simanzi na pigo kwetu.”

Naye Jonas Hamsin, alisema mbunge huyo alikuwa rafiki wa kila mtu jimboni hapo na kusaidia kila sehemu ya maendeleo na kwamba kwa sasa wanafikiria ujenzi aliokuwa ameanzisha wa ofisi ya CCM kata utaishia wapi, lakini miradi mingine ikiwamo Shule ya Sekondari Mwale.

"Katika ahadi zake wakati wa kampeni ametekeleza kwa kiasi kikubwa, japokuwa kuna maeneo mengine alikuwa hajakamilisha kama ujenzi wa ofisi ya chama kata na Shule ya Sekondari Mwale ambayo haijakamilika, kwa ujumla tumepoteza mtu muhimu," amesema Hamsin.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kata ya Chimala, Yusuph Kiswaga alisema kuondokewa na kiongozi huyo imeacha pengo kubwa kutokana umahiri wake na ushirikiano aliokuwa nao katika kupambania maendeleo ya wananchi.

"Sisi Chadema tunasikitika sana alikuwa mtu mwema kwa jamii nzima, alipambana kuwapigania wananchi ikiwamo lile sakata la hifadhi baada ya askari kuvamia maeneo na kujeruhi watu, tumebaki na huzuni na ni pengo kubwa kwetu na jimbo kwa ujumla" alisema Kiswaga.

Mbunge wa viti maalumu wazazi Taifa, Bahath Ndingo alisema mbunge Mtega alikuwa mzazi na mlezi kwa Wilaya ya Mbarali akieleza kuwa mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa Juni 10 alipompa pole ya kuondokewa na mdogo wake akimuandikia mistari ya biblia.

"Hata tukiwa bungeni au kukutana popote sikumuita mheshimiwa au jina gani zaidi ya Baba, kwa sababu alikuwa mfano wa mlezi, ni pigo kwa Taifa kutokana na maisha aliyoishi ikiwamo kuwapambania wananchi kwenye mambo ya maendeleo," alisema Bahath.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live