Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Neema ya umeme yanukia wateja 44,000 Kigamboni

2c7d3070d5d72a11f38f03baa4a0cfd8.png Neema ya umeme yanukia wateja 44,000 Kigamboni

Fri, 29 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MRADI wa ujenzi wa kituo cha Dege cha kupoza na kusambaza umeme wa gridi wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam, uko mbioni kukamilika na utazinduliwa Februari 28, mwaka huu ili kuwanufaisha wateja zaidi ya 44,500.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo juzi jijini Dar es Salaam na Mradi wa Kinyerezi II, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato alisema mradi huo utakapokamilika utaondoa kero na adha ya kukatika kwa umeme kunakosababishwa na hitilafu mbalimbali.

Byabato alisema Wilaya ya Kigamboni kwa sasa haina umeme wa gridi, bali umeme wa msongo wa 33 unaotoka wilaya za Ilala na Temeke na kwamba kwa kuwa umeme huo unatoka mbali, mara kadhaa hutokea hitilafu na kukatika.

Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa gharama ya Sh bilioni 26 na umesimikwa minara 78 na kuwa na laini sita za umeme mkubwa ambao ukikamilika awamu ya kwanza utazalisha megawati 48 na kwamba kwa sasa mahitaji ya umeme katika mji huo ni megawati 18.

“Ni kweli Kigamboni haina umeme wa gridi, unapata umeme kutoka Temele na Ilala umbali mrefu sasa mradi huu wa Dege unakamilika Februari hii na nimewaagiza Tanesco, kuhakikisha Februari 28, mwaka huu mradi huu unazinduliwa ili kuondoa adha na viwanda sasa vipate nishati ya uhakika vifanye kazi,” alisema Naibu Waziri.

Mbali na maagizo hayo, Naibu Waziri pia aliiagiza Tanesco kuangalia vigezo vinavyotakiwa kama Kigamboni inavyo ili utangazwe kuwa mkoa wa Kitanesco kwa lengo la kurahisisha huduma karibu kwa wananchi na wadau wengine.

Awali akizungumzia changamoto za Kigamboni, Mkuu wa wilaya hiyo, Sara Msafiri alisema hakuna umeme wa uhakika kwa sababu wanategemea umeme kutoka Mbagala wilayani Temeke na laini nyingine kutoka Ilala na kuwa endapo itatokea hitilafu Ilala, Kigamboni huwa giza.

“Tuna changamoto ya ukosefu wa umeme wa uhakika, kwa sasa tunapata umeme wa msongo wa 33 kutoka Temeke laini moja na nyingine inatoka Ilala, sasa kama huko kwenye chanzo kuna hitilafu basi ujue na sisi huku tunaathirika na wakati mwingine umeme unafika lakini haina nguvu kwa sababu unatoka mbali na wakati mwingine unapotea njiani,” alisema Msafiri.

Alisema changamoto hiyo ilisikika kwa Rais John Magufuli kutoa fedha Sh bilioni 26 ili kutekeleza mradi huo kujenga kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Dege ambao kwa sasa umefika zaidi ya asilimia 92 kwa mradi kukamilika.

Akizungumzia mahitaji ya umeme Kigamboni, Meneja Tanesco wa eneo hilo, Ramadhan Bilal alisema hivi sasa Kigamboni ina jumla ya wateja 44,500 na kati ya hao wateja 44,200 ni wadogo, viwanda vikubwa viko 11 na viwanda vidogo viko 90 na kwamba wateja wakubwa wana changamoto ya umeme kwa kuwa uliopo ni mdogo hauna nguvu.

“Ingawa mahitaji ya umeme Kigamboni ni megawati 18 na sasa tunazo hizo megawati, ila wateja wakubwa hawawezi kuutumia kwa kuwa hauna nguvu, tunautoa mbali unakutana na changamoto za njiani na unafika hauna nguvu, lakini kukamilika kwa Mradi wa Dege utamaliza tatizo,” alisema Bilal.

Alisema kwa sasa Tanesco kwa mwezi Kigamboni inakusanya mapato ya Sh bilioni 3.8 kutoka kwa wateja wao na hiyo ni moja ya kigezo cha wao kufanywa Mkoa wa Tanesco kwani hata idadi ya wateja ni kubwa na sasa wako takribani wateja 44,500.

Awali akizungumzia mradi huo, Msimamizi wa Mradi wa Dege kutoka Tanesco, Neema Mushi alisema uko kwenye hatua za mwisho na mkandarasi anaendelea kufunga vifaa na kusimika nguzo kubwa zilizosalia ili ifikapo Februari mradi uwe umekamilika.

Akiwa katika Mradi wa Kufua Umeme wa Kinyerezi, Naibu Waziri alijionea mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi asilia ukiendelea na kujulishwa kuwa upanuzi wa Mradi wa Kinyerezi I unaendelea baada ya kumpata mkandarasi mpya kutokana na mkandarasi wa awali kufilisika.

Mradi huo ni wa kuzalisha megawati 185 zitakazounganishwa kwenye Gridi ya Taifa na kuwa mradi huo una thamani ya Dola za Marekani milioni 188 na unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa fedha za ndani.

Chanzo: habarileo.co.tz