Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndugu 7 waliokufa ajalini Singida wazikwa

955fbe1dfe2ac1527c10bc2175d6ea2f Ndugu 7 waliokufa ajalini Singida wazikwa

Thu, 17 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella ameongoza waombolezaji kuaga miili ya saba, kati ya tisa, waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea mwishoni mwa wiki wakielekea harusini mkoani Singida. Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya hiace na lori la mafuta, ambayo yaligongana.

Watu hao saba walizikwa jana katika makaburi ya Mabatini jijini Mwanza. Mmoja alisafirishwa kwenda kuzikwa Bukoba, Kagera na mwingine alikwenda kuzikwa wilayani Magu.

Akizungumza kwenye maziko hayo, Mongella alisema mkoa umepata pigo kubwa kwa kuondokewa na watu saba.

Aliomba familia ya marehemu, wawe na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu. Pia alisema serikali ipo pamoja nao kwenye kipindi hiki cha maombolezo.

Mama wa watoto saba waliopoteza maisha katika ajali hiyo ya gari lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Singida, Aisha Mayunga aliomba serikali imsaidie msaada katika kipindi hiki kigumu cha msiba.

Mkazi huyo wa Mtaa wa Mabatini alisema wanawe hao saba, walikuwa wanakwenda kwenye harusi katika eneo la Itigi mkoani Singida na walipoteza maisha kwenye ajali hiyo.

Mama huyo alisema ajali hiyo ilihusiha msafara wa watu 19. Alisema wanae wawili ndiyo waliosalimika katika ajali hiyo.

Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya hiace, yenye namba T754CGS, iliyokuwa ikitokea Mwanza na lori la mafuta namba T423BRG yenye trela namba T384 BYE, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Kahama mkoani Shinyanga.

Mayunga aliwataja wanawe wawili waliosalimika katika ajali hiyo ni Elly Mayunga, ambaye ni bwana harusi na binti yake, Shakila Mayunga aliyekatika mguu.

Shehe wa Wilaya ya Nyamagana, Othman Ndaki aliwataka wanafamilia hao kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha kupoteza ndugu zao.

“Ndugu zangu nawaomba wote muwe na subira katika kipindi hiki kigumu cha kupoteza wapendwa wenu, kwani hayo yote ni mapenzi yake Mungu,” alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike, ajali hiyo ilitokea Kijiji cha Mkiwi, Ikungi Singida na kuua watu 14 na kujeruhi wengine 13.

Baadhi ya waombolezaji waliofika kuhani msiba huo, walisema kuna haja ya askari wa usalama barabarani, kuendesha msako wa kuwabaini madereva wazembe ili kuzuia matukio ya ajali za namna hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz