Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndugai apigania lami mji mdogo Kibaigwa

354aa841d0f8c922c7368b5031b9ad5e Ndugai apigania lami mji mdogo Kibaigwa

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE wa Kongwa ambaye pia ni Spika wa Bunge, Job Ndugai ametaka mji mdogo wa Kibaigwa kukumbukwa na kuanza kupata barabara za lami.

Alisema hayo jana wakati akizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara.

Alisema tangu mji mdogo wa Kibaigwa kuanzishwa haujawahi kupata hata futi moja ya barabara yenye lami.

Aidha alimtaka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura), kutenga fedha kwa ajili ya mji wa Kibaigwa.

“Tarura haijawahi kutenga fedha zozote kwenye mji wa Kibaigwa. Kibaigwa haijawahi kupata hata futi moja ya barabara ya lami, tuanzie hata kilomita tatu au nne watu hao wamekosa fursa kwa muda mrefu,” alisema.

Aliitaka Tarura kuonesha ushahidi wa maandishi kama waliwahi kutenga fedha kwa ajili ya barabara za Kibaigwa na barabara hizo hazikupata fedha.

“Mniambie tu tulipeleka maombi lakini Kibaigwa ilikatwa ili nimjue huyo anayeiondoa Kibaigwa kila mwaka ili isipate fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara,” alisema

Pia, alitaka kuangaliwa uwezekano wa barabara kutoka Narco hadi Kongwa kujengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri wa watu wanaokwenda Kongwa.

Alisema kuanzia Kongwa Mbuyuni hadi Narco hakuna fidia yoyote ambayo italipwa kwa wananchi kwani eneo lote lile ni la serikali.

Alisema wilaya ya Kongwa imekuwa na changamoto nyingi za barabara mbovu huku baadhi ya madaraja yakiharibika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha msimu uliopita.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda alitaka kuwekwa kwa taa za barabarani eneo la Bahi.

“Tumepoteza askari polisi wawili, barabara kuu pale Bahi Mjini haina taa, juzi kuna askari mmoja amegongwa na kufariki usiku sababu tu eneo lile ni giza na hakuna taa,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Sezeria Makota alitaka kuimarishwa kwa barabara za vijijini ili wananchi wanaosafirisha mazao wafike kwenye masoko kwa wakati. “Tunaomba tupate fedha kwa ajili ya barabara za Kondoa Vijijini,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alitaka kuwe na mpango mkakati wa ujenzi na ukarabati wa barabara..

“Pamoja na kutenga fedha lakini hata madaraja yawe yanajengwa kwa viwango mengine yakipitiwa na mvua tu yanaharibika tabu inarudi pale pale, ushirikishwaji wa wananchi ni mzuri wakati wa ujenzi kwani wana historia na maeneo yao,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz