Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndoa za utotoni tishio Longido

Ndoa Utotoniiiii.jpeg Ndoa za utotoni tishio Longido

Fri, 9 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati wanaharakati wa kutetea haki za wanawake na watoto wakiwa katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mwaka 2022 ambazo zitahitimishwa Desemba 10, ndoa za utotoni bado ni changamoto kubwa katika jamii za kifugaji nchini, ikiwamo wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha.

Watoto wadogo wenye umri chini ya miaka 15 bado wanaolewa kwa kasi, hivyo kuathiri ndoto za maisha yao, ikiwemo kupata haki ya kusoma na wengi wakiishia kufanyiwa ukatili maishani mwao.

Lipo tukio la Septemba 22 mwaka huu, lililohusisha mtoto Mesoni Kashiro (15) mkazi wa kijiji cha Gilailumbwa, kujeruhiwa kwa kipigo na mumewe Namendea Lesiria kwa kosa la kumwaga dawa ya mifugo.

Tukio hilo lilivuta hisia za watetezi wa haki za watoto kutaka uchunguzi wa kukomeshwa ukatili huu, lakini kumbe tatizo ni kubwa zaidi na sio kwa Mesoni tu.

Pamoja na nchi kupiga kelele na kuzua mijadala ya hapa na pale kuhusu ndoa za utotoni na ukatili wanaofanyiwa watoto hao baada ya kuolewa, tatizo katika jamii za pembezoni bado ni kubwa na linahitaji juhudi za pamoja kuwanusuru.

Mkurugenzi wa shirika la kusaidia watoto na wanawake katika jamii za kifugaji la Mimutie Women Organization (MWO), Rose Njilo anasema ukatili dhidi ya watoto umekithiri katika jamii za kifugaji na ni jambo linalopaswa kushughulikiwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali.

“Hili ni tatizo kubwa, watoto wadogo wanalazimishwa kuolewa na kwa kuwa hawana uwezo wa kukataa, wanaozeshwa na kufanyiwa ukatili mkubwa na hawana watetezi,” anasema.

Anasema shirika lake karibu kila mwezi linapokea kesi za watoto kuolewa na wengine kukimbia makazi, kutokana kulazimishwa kuingia kwenye majukumu ya ndoa wakiwa na umri mdogo.

“Hii kesi ya Mesoni ni mfano tu wa matukio ya ukatili, lakini hadi sasa nina watoto saba walifanyiwa ukatili wa ndoa hizi za utotoni,” anasema.

Uchunguzi uliofanywa katika vijiji vya Olbomba, Kimokowa, Engarenaibo umebaini kati ya kaya 10, kaya 4 kuna watoto wadogo wameolewa katika wilaya ya Longido na hali hii ipo pia hata katika wilaya za Monduli, Ngorongoro, Kiteto na Simanjiro.

Ndoa hizo zinaendelea kuwepo licha ya uwepo wa sheria kuzuia, Serikali kutoa elimu na asasi za kiraia kupinga kuendelea kwa ndoa hizi.

Akizungumzia hali hiyo, Mchungaji Musa Murdoko wa Kanisa na Baptist Longido anasema ndoa za utoto bado ni changamoto kubwa.

“Hili jambo lina mshikamano mkubwa na mila na sisi kama viongozi wa dini tunatoa elimu sana lakini watu wamegoma kubadilika,” anasema. Anasema tatizo hili linachangiwa na umaskini na viwango vidogo vya elimu, kwani familia hutegemea mifugo tu katika maisha ya kila siku.

“Utakuta binti mdogo anaolewa bila ridhaa yake lakini kutokana na kuwaheshimu wazazi na viongozi wa mila hawezi kupinga,” anasema.

Kauli ya halmashauri Ofisa maendeleo ya jamii wilayani Longido, Grace Mghase anasema ndoa za utotoni bado ni changamoto katika wilaya hiyo.

Anasema elimu inaendelea kutolewa, lakini changamoto ni utayari mdogo wa familia kuachana na ndoa hizi za utotoni.

“Wanabadilika kwa kasi ndogo sana, ila tunaendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na wadau wengine wa asasi zisizo za kiserikali,” anasema Grace.

Naye Debora Makando, Ofisa jinsia na miradi wa Shirika la kusaidia jamii za pembezoni la MAIPAC, anasema ndoa za utotoni ni ukatili ambao ni changamoto kubwa katika jamii za pembezoni.

“Bado tunaomba ushirikiano mkubwa wa Serikali na wadau wengine katika kusaidia jamii hizi za pembezoni kuachana na mila zilizopitwa na wakati,” anasema.

Msimamo wa Serikali Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima anasema jamii inapaswa kukomesha ukatili wa ndoa za utotoni kuanzia kwenye ngazi ya familia.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuwafanyia ukatili watoto wadogo, ikiwepo kuwaoa wakiwa chini ya umri stahiki, kuwafanyia vitendo vya ubakaji na udhalilishaji,” anaonya Gwajima.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa shirika la kusaidia ustawi wa wanawake na watoto (WOCWELS), Mary Mushi anasema changamoto kubwa ya ndoa za utoto ni sheria ndio sababu ameamua kupeleka kesi mahakamani kutetea umri wa kuolewa uwe kuanzia miaka 18.

Anasema sheria ya ndoa ina mapungufu, kwani bado inatoa haki, mtoto mdogo kuolewa kwa ridhaa ya wazazi wake.

Chanzo: Mwananchi