Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nditiye atoa wiki 3 treni Moshi- Arusha

Fbf19013f17be2303a03e180fef99f50 NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye

Thu, 16 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, ametoa siku 21 kwa uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), kuhakikisha usafiri wa reli ya Moshi-Arusha unarejea ili kurahisisha usafiri wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Ametoa agizo hilo baada ya kusafiri kwa kutumia kiberenge kati ya Moshi na Arusha, kwa lengo la kukagua reli hiyo kabla usafiri wa treni haujaanza.

Amesema usafiri wa treni ya Moshi-Arusha ni muhimu kwa wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ili waweze kusafirisha mizigo kwa treni na kuwapunguzia gharama za usafirishaji.

“Natoa siku 21 kwa Latra na TRC kuhakikisha ndani ya muda huo ukarabati wa treni ya Moshi na Arusha unakamilika ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya usafiri kwa shughuli za biashara na kawaida,’’ alisema.

Aidha, Nditiye aliwataka wananchi kulinda miundombinu ya reli na kuacha kufanya shughuli za kilimo karibu na reli, kuchunga mifugo na kupita hovyo na boda boda wakati treni ikiwa inapita, kwani ni kosa kisheria. Kaimu Mkuu wa Usalama wa Reli na Ulinzi wa TRC, Adolphine Ndyetabuta, alisema watatekeleza maagizo ya Naibu Waziri ndani ya muda alioutoa ili usafiri wa treni uanze bila kipingamizi chochote.

Aliwataka wananchi kushirikiana na shirika hilo kulinda na kuwafichua wanaopinga jitihada za Rais John Magufuli za kuboresha huduma ya usafiri wa reli, kwani usafiri huo kwa asilimia kubwa unatumiwa na wananchi wanyonge na wenye kipata cha chini.

Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe, alisema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na TRC inaandaa kutoa elimu kwa jamii kwa lengo la kuwataka wananchi kuacha kuikimbilia treni inapokuwa ikifanya safari zake katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ili kuepuka ajali.

TRC ilisitisha huduma ya usafiri wa treni kati ya Moshi na Arusha kwa zaidi ya miaka 18 sasa, hivyo kuanza tena kwa huduma hiyo, itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi hususani wa kipato cha chini na kati.

Chanzo: habarileo.co.tz