Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tamisemi, Deogratius Ndejembi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako, Kenneth Haule kuhakikisha mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Kitandililo, anaongeza kasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Ndejembi ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kutembelea ujenzi wa shule hiyo mkoani Njombe, ambayo ujenzi wake unagharimu Sh683 milioni kupitia mradi wa 'SEQUIP.'
Akizungumza na viongozi na wananchi wa Kata ya Kitandililo, Ndejembi ameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo na amemtaka mkandarasi kujenga usiku na mchana, kuongeza idadi ya nguvu kazi ili kutimiza malengo ya Serikali ya kukamilisha ujenzi huo ifikapo Oktoba 31 mwaka huu.
"Nimesikitishwa na kasi ya ujenzi wa shule hii, nchi nzima mwisho wa ujenzi huu ni Oktoba 31 na mimi sitobadilisha muda huo uliopangwa. Nikuagize Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha mnambana mkandarasi ili aongeze nguvu kazi," amesema.