Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndege vita zatikisa anga maandalizi ya Uhuru Tanzania

Ndege vita zatikisa anga maandalizi ya Uhuru Tanzania

Fri, 6 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Kama yupo mkazi wa jiji la Mwanza nchini Tanzania ambaye wiki moja iliyopita hakufahamu kuwa jiji hilo ndilo mwenyeji wa maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru ni dhahiri sasa anafahamu.

Uhakika wa ufahamu huo unatokana na mambo na matukio kadhaa, moja wapo ikiwamo misafara ya magari madogo na mabasi kadhaa yaliyosheheni Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Askari wa Jeshi la Polisi pamoja na wenzao wa Magereza.

Lakini kubwa kuliko ni mirindimo na vishindo vya miungurumo ya ngege jeshi zinazopita kwa kasi katika anga la jiji la Mwanza kuanzia mwanzoni mwa wiki hii.

Pamoja na vishindo na miungurumo ya ndege jeshi, wakazi wa jiji la Mwanza pia wanashuhudia maonyesho ya kijeshi ya helkopta zinazokatiza angani kwa kasi huku askari wakiwa wamening’inia kwa kamba.

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya maandalizi ya sherehe za miaka 58 ya Uhuru anayesimamia hamasa na burudani, Nyakia Ally anasema maonyesho hayo ya kijeshi ni kati ya matukio ya kipekee ambayo hajawahi kushuhudiwa kabla yatakayopamba maadhimisho ya mwaka huu.

“Hayo ya helkopta wanazoning’inia askari na miungurumo mikubwa ya ndege vita zinazopita angani kwa kasi ni sehemu tu ya maonyesho ya na burudani za kipekee zitakazokuwepo kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru,” anasema Nyakia

Pamoja na maonyesho ya kawaida ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama ambayo yanaendelea na mazoezi, Nyakia anasema maadhimisho ya mwaka huu pia yatahusisha maonyesho ya walinzi wa jadi maarufu kama sungusungu zaidi ya 1, 500.

Maonyesho ya halaiki yanayotolewa na vijana wa chipukizi kutoka mikoa yote nchini yalitozoeleka katika maadhimisho ya kitaifa pia yatakuwepo mwaka huu, lakini ikiwa na vionjo tofauti.

“Chipukizi watafanya maonyesho yao yaliyozoeleka ikiwemo kuchora maumbo, ramani na bendera ya Taifa wakitumia miili yao; lakini pia kutakuwepo mambo mengine ya ziada kuwaburudisha Watanzania watakaohudhuria na walioko mbali watakaofuatilia maadhimisho hayo kwa njia ya Luninga,” anasema Nyakia

Burudani ya ngoma za asili, muziki wa kizazi kipya pamoja na nyimbo maalum kutoka kwaya za AIC Makongoro ya jijini Mwanza na Tanzania One Theater (TOT) pia zitakuwepo.

Akizungumzia maandalizi ya maadhimisho hayo, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mangella amesema kila kitu kinaenda jinsi kilivyopangwa na kuwasihi wakazi wa mkoa huom hasa jiji la Mwanza kujitokeza kwa wingi kuhudhuria maonyesho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya CCM Kirumba.

“Mwanza tuko tayari na tutayafanikisha maadhimisho ya Kitaifa ya miaka 58 ya Uhuru kama tulivyofanya kwa yale ya siku ya Ukimwi duniani,” amesema na kutamba Mongella

Halmashauri ya jiji la Mwanza kwa kushirikiana na wadau wengine nao hawako nyuma katika maandalizi hayo kwa kuimarisha usafi mitaani ikiwemo kuondoa vibanda na wafanyabishara wadogo maarufu kama wamachinga waliojenga na kutandaza bidhaa zao katika njia za waenda kwa miguu na juu ya mifereji ya maji machafu.

Chanzo: mwananchi.co.tz