Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nchi 26 zinashiriki mjadala wa misitu Tanzania leo

Saohilllls Nchi 26 zinashiriki mjadala wa misitu Tanzania leo

Sat, 13 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

NCHI 26 ni miongoni mwa wadau zaidi ya 400 waliothibitisha kushiriki kongamano la uwekezaji katika sekta ya misitu litakalofanyika kwa siku tatu Mjini Mafinga wilayani Mufindi, kuanzia leo.

Kongamano hilo linalofanyika kwa mara ya kwanza nchini, litazinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa likilenga kuchochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji katika sekta hii ya misitu mkoani Iringa na nchini kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga alisema mbali na nchi hizo 26, kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na baadhi ya mabalozi na wawakilishi wao.

Alisema kupitia kongamano hilo, wadau waliojitokeza wataonesha bidhaa mbalimbali wanazozalisha kupitia malighafi za miti, matumizi ya teknolojia katika kuendeleza sekta hiyo, historia na uzoefu wa upandaji miti.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Saad Mtambule alisema wilaya hiyo ndiyo yenye mashamba makubwa ya miti kuliko nyingine nchini, ikiwa na ekari zaidi ya 220,000 za miti ya kupandwa.

Alisema kufanyika kwa kongamano hilo wilayani hapo kunatarajia kuibua zaidi fursa mbalimbali zinazoweza kufanywa kupitia sekta hiyo ya misitu na hivyo kutoa mchango stahiki katika uchumi wa taifa.

Mtambule alisema jukumu kubwa ni kurahisisha mazingira ya uwekezaji kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza.

Baadhi ya wadau wamepongeza kufanyika kwa kongamano hilo wakisema litasaidia kuainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo na kuwekewa mikakati ya kuzishughulikia.

Meneja wa Kiwanda cha karatasi cha MPM Mgololo, Gregory Chogo alizungumzia barabara ya Mafinga-Mgololo yenye urefu wa kilometa 85 akiomba ijengwe kwa kiwango cha lami kurahisisha usafirishaji wa malighafi na bidhaa wanazozalisha na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji.

Mwakilishi wa Kampuni ya Saohill Industries na Green Resources Ltd, Isack Shirima alisema uzalishaji holela wa mazao ya miti wilayani humo umesababisha viwango vya ubora wa bidhaa hizo kupata changamoto ya masoko katika masoko mengi ya ndani na ya kimataifa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wavunaji Miti Saohill (UWASA), Christian Aia aliiomba serikali kupitia upya na kuzifanyia marekebisho tozo katika malighafi miti inayouzwa katika misitu ya serikali kwani ni kilio kikubwa kwa wawekezaji.

Mkulima mkubwa wa miti wilayani humo, Matekeleza Chang'a alisema endapo serikali itapunguza tozo katika miti yake, itakuwa imesaidia kupunguza kasi kubwa ya uvunaji miti michanga katika mashamba binafsi kwa sababu ya udogo wa bei yake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live