Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Naibu Waziri aitaka Takukuru ikachunguze uongo Bandari ya Lindi

29466 Tanga+pic TanzaniaWeb

Fri, 30 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuatilia na kuchunguza thamani ya fedha zilizotumika kujenga gati ya Bandari ya Lindi.

Kampuni ya Comfix & Engineering Ltd ndiyo inayotekeleza mradi huo ambao ulitakiwa kukamilika kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Mei mwaka 2015, gharama yake ni Sh3.5 bilioni na mpaka sasa tayari mkandarasi amelipwa Sh2.44 bilioni.

Nditiye ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati ya Bandari ya Lindi mkoani humo ambapo amebainisha kasi ya utendaji kazi kwenye gati hilo hairidhishi.

“Kazi ni ya mwaka mmoja ila imechukua miaka mitatu hadi sasa na bado haijakamilika, Naielekeza Takukuru waje wafuatilie thamani ya fedha zilizotumika kujenga gati hili,” amesema Nditiye.

Taarifa ya wizara hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo Alhamisi imemnukuu Nditiye akisema miradi ya maendeleo ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inayotekelezwa nje ya Bandari ya Dar es Salaam haitekelezwi ipasavyo.

“Tufike mahala tuheshimu fedha za Serikali na za wananchi, TPA hamfiki eneo la mradi wakati wa kuandaa nyaraka na hata ujenzi wa miradi husika inavyoendelea hivyo tunaingia hasara,” amesema Nditiye.

Nditiye pia ametoa rai kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dk Phillip Mpango kuwachukulia hatua watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Lindi wanaosimamia Bandari ya Lindi kwa kuikosesha Serikali mapato kwa kuwasaidia wafanyabiashara kukwepa kodi na kuvusha biashara za magendo.

“Wafanyakazi wa TRA waliopo Bandari ya Lindi wameoza, Waziri wa Fedha na Mipango tafadhali safisha uozo huo kwa kuwa wamepitisha madumu ya mafuta 650 mwezi huu (Novemba) yaliyopakiwa Zanzibar na kushushwa Lindi yakiwa madumu 30 tu na kusema kuwa yako tupu,” amesema Nditiye.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilayani humo wanapambana kudhibiti bandari bubu zilizopo na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wasio waaminifu wanaokwepa kodi.



Chanzo: mwananchi.co.tz