Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Naibu Waziri Mgumba ataka vijiji vitenge ardhi kuajiri vijana

Tue, 4 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rufiji. Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba amezitaka Halmashauri za wilaya nchini kutenga ardhi kwa ajili ya vijana kujiajiri katika sekta ya kilimo.

Mgumba ameyasema hayo leo Jumatatu Juni 3, 2019 katika kijiji cha Mkongo wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, alipokuwa akifunga mafunzo ya kilimo kwa vijana yanayotekelezwa na Ushiria wa Wahitimu wa Chuo kikuu cha Sokoine (Sugeco), ambapo amesema halmashauri zinapaswa kuviagiza vijiji kutoa ardhi.

"Tunaposema halmashauri za wilaya zitenge ardhi, je wanayo? Mimi nimetoka huko vijijini, ardhi inamilikiwa na vijiji. Haya maelekezo tuyashushe kwa vijiji, ni wananchi wenyewe kupitia mikutano watenge ardhi za vijana," amesema.

Mgumba pia ameziagiza Halmashauri kutenga asilimia 10 za kina mama, vijana na wenye walemavu, ili kutimiza adhima ya Serikali ya kutoa ajira kwa vijana.

"Halmashauri ziwe na matumizi ya vijana ili wapate mafunzo yatakayowawezesha kujiajiri. Kituo hiki kiende na mikoa mingine, Serikali ilianza hilo tangu 2006, tulitoa maelekezo kila kata iwe na kituo cha mafunzo ya vitendo vya Kilimo. Hilo halikufanyika vizuri, wengine wamebadilisha matumizi," amesema.

Kuhusu maonesho ya wakulima ya Nanenane, Mgumba amesema yameanza kupoteza mwelekeo kwa kuwa yananufaisha watumishi wa umma kuliko wakulima wenyewe.

Pia Soma

"Yale maadhimisho ya Nanenane huwa yanawasaidia watumishi wa Kilimo, sio wakulima wenyewe. Ndio maana tunataka yashuke huko chini. Maadhimisho yawepo lakini twende mbali zaidi kwa kupeleka mafunzo ya vitendo kwa wakulima.

Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Mkurugenzi wa Sugeco, Revocatus Kimario amesema jumla ya vijana 58 wamehitimu mafunzo hayo ya siku 14 yakiwa katika awamu tofauti za miezi minne.

"Tangu tulipoanza mafunzo mwaka 2015 tumeshafundisha vijana 850. Mbele yako ni vijana 58 wakitoka mikoa ya Singida, Dodoma, Morogoro na Pwani wamejifunza kwa vitendo kwa asilimia 80 na nadharia kwa asilimia 20 ya kilimo na ufugaji," amesema Kimario.

Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Fred Kafeero amesema mradi huo ni kielelezo cha shirika hili na  Serikali kupambana na tatizo la ajira kwa vijana.

"Vijana wanaendelea kuongezeka na changamoto zinajitokeza kwa nchi zinazoendelea. Fursa zinajitokeza, vijana wana uwezo wa kuchangia uchumi vijijini.FAO inasaidia maendeleo ya vijana wa vijijini kikiwa pamoja na changamoto za vijana kupata kazi za hadhi.

Amesema kupitia miradi kama hiyo Fao imeshawasaidia vijana zaidi ya 17,000 nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz