Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Naibu Waziri Mgalu awanyooshea kidole Tenesco

12013 TANESCO+PIC TanzaniaWeb

Mon, 23 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetakiwa kuhakikisha watu wanaolipia kuunganishiwa umeme wanapatiwa huduma hiyo ndani ya muda mfupi.

Agizo hilo limetolewa leo Julai 23, 2018 na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alipotembela miradi mbalimbali iliyopo Kanda ya Dar es Salaam na Pwani.

Mgalu ametoa agizo hilo kufuatia kuwepo kwa malalamiko mengi ya watu ambao wamelipa fedha Tanesco kwa ajili ya kuunganishiwa umeme lakini hilo halijafanyika.

Amesema ni jambo la kushangaza Serikali kudaiwa na wananchi kupitia Tanesco wakati fedha hizo zingetumika kufanya mambo mengine.

Mgalu amesema amepata malalamiko mengi kutoka kwa watu waliolipia fedha kwa ajili ya kuunganishiwa umeme lakini hadi sasa hawajapata huduma hiyo.

"Hili suala halivumiliki na Serikali ya awamu ya tano tumejipanga kuhakikisha watu wanapata umeme, sasa kitendo cha wao kupata mwamko na kulipia halafu Tanesco mnatuangusha naomba ifike mwisho," amesema Mgalu na kuongeza:

"Nataka kufikia Septemba 30 kusiwepo na malalamiko ya aina hii tena kwa sababu sioni kinachowakwamisha kama ni manunuzi yamesharudi ngazi ya kanda."

Mgalu amesema, “nichukue fursa hii kuwaomba radhi wananchi wote waliokutana na kadhia hii, Serikali iko pamoja nanyi lengo letu mpate umeme."

Amesema hatua ya Serikali kurudisha manunuzi ya vifaa vya kuunganishia umeme kwa ngazi ya kanda ni kutaka kupunguza mlolongo wa upatikani wa huduma hiyo.

Akielezea kuhusu hilo Meneja mwandamizi wa Tanesco kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi Mahende Mugaya amesema changamoto kubwa iliyopo ni upatikanaji wa nguzo.

Amesema kuanzia Januari kanda yake ina maombi zaidi ya 5,000 ya watu ambao wanahitaji kuunganishiwa umeme na tayari wamelipia.

"Kinachotusumbua ni nguzo ila tunajitahidi kadri ya uwezo wetu kuwasiliana na wasambazaji watuletee za kutosha," amesema na kuongeza:

“Niwaahidi wote waliolipia umeme kuanzia Januari hadi Juni 30 muda si mrefu wataunganishiwa."

Chanzo: mwananchi.co.tz