Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NSSF ilivyojisogeza karibu na wadau wake Temeke

096b8d883379f0c18e62823674c68f80.png NSSF ilivyojisogeza karibu na wadau wake Temeke

Mon, 28 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Godwin Gondwe, kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali aliendesha kampeni iliyopewa jina la ‘One Stop Jawabu’ ambayo ilifanyika katika maeneo mawili ya Mbagala Zakhem na Tandika Mwembe Yanga.

Nia ya kampeni ya ‘One Stop Jawabu’ ilikuwa ni kusogeza karibu huduma za taasisi hizo za umma kwa wananchi ambao walifika na kujipatia taarifa na huduma mbalimbali walizohitaji. Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazoshiriki kampeni hiyo kwa kupokea changamoto mbali mbali za wananchi katika Wilaya ya Temeke.

Meneja wa NSSF Mkoa wa Temeke, Rebule Maira anasema kupitia maonesho hayo, shirika linasikiliza na kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili wanachama wake wanaofika katika banda lao na kuzipatia ufumbuzi ikiwa ni mpango wa serikali na shirika hilo wa kusogeza huduma karibu na wananchi.

Maira amesema katika kutekeleza majukumu manne ya shirika ambayo ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao, kupitia maonesho hayo NSSF inaandikisha wanachama wapya kutoka sekta rasmi na sekta isiyo rasmi wakiwemo wakulima, wavuvi, wafugaji, mamalishe na bodaboda.

Pia inatoa elimu mbalimbali kuhusu mafao yanayotolewa na shirika hilo pamoja na kufanya uhakiki wa taarifa za wanachama wastaafu na wategemezi wao ili ziwekwe kwenye kumbukumbu sahihi. “Kama mnavyofahamu baada ya mabadiliko ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii, sasa NSSF inahusika na watu waliopo katika sekta rasmi na sekta isiyo rasmi, hivyo kupitia maonesho haya tunahudumia makundi yote haya,” anasema.

Anasema kwa watumishi waliopo katika sekta rasmi wanaotembelea banda la shirika hilo watapata nafasi ya kuangalia michango yao kama inapelekwa na mwajiri wake na kupata taarifa zinazohusu mafao na huduma nyingine zinazotolewa na NSSF. Maira anasema NSSF imeweka lengo la kufikisha huduma zake kwa wananchi wote, na kwamba kwa wanachama wastaafu watapata fursa ya kuhakiki taarifa zao ambazo zitawekwa katika kumbukumbu sahihi za shirika hilo ili waendelee kupokea mafao yao pasipo mkwamo wowote.

Anasema NSSF itaendelea kuwasaidia wananchi wa kawaida kwa kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kujiunga na shirika hilo ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa yakiwemo ya urithi, uzazi na mirathi.

“NSSF inawaelimisha wananchi, inawaandikisha ili wananchi hawa wanufaike na huduma za hifadhi ya jamii,” anasema. Meneja huyo anasema shirika hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (SIDO), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) pamoja na Benki ya Azania wataanza kutoa mikopo kwa wajasiriamali ili iwasaidie kuongeza mitaji yao. Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliotembelea banda la NSSF kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali wametoa ushuhuda namna shirika hilo linavyotatua changamoto zao ambazo kwa muda mrefu zilikosa majibu.

Mjane Kudra Fumagwa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kupitia NSSF kwa namna inavyotatua changamoto zinazowakabili wananchi wa hali ya chini ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli ambaye amejipambanua kuwatetea wanyonge.

“Naishukuru sana serikali kupitia NSSF kwa namna inavyotatua changamoto hasa zinazotukabili sisi wajane na wananchi wote wa hali ya chini, siamini kama tatizo langu lingepatiwa ufumbuzi, nasema asanteni sana NSSF,” amesema Kudra.

Anasema alikuwa anafuatilia madai ya mafao ya aliyekuwa mumewe, lakini baada ya kufika katika banda la NSSF shida yake imepatiwa ufumbuzi kwa haraka, na ameridhika na huduma zinazotolewa kwa wanachama wa shirika hilo.

Kudra anawaomba wananchi wenye shida mbali mbali kutembelea katika maonesho hayo ili wapate ufumbuzi wa matatizo yao, huku akiwataka kupita kwenye banda la NSSF ili wapate elimu na wajiunge na shirika hilo kwa ajili ya kujiwekea akiba yao ya baadaye. Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Gondwe anaipongeza NSSF kwa juhudi zake za kutatua kero zinazowakabili wanachama wake pamoja na kuwaelimisha wananchi waliopo katika sekta isiyo rasmi ili wanufaike na hifadhi ya jamii baada ya kujiandikisha na shirika hilo.

Kwa upande wake, Thomas Richard ambaye ni Katibu wa Kikundi cha Kivulini Youth Network, anawaomba wenye vikundi kuwaandikisha wanachama wao NSSF ili wanufaike na huduma zinazotolewa na shirika hilo ikiwemo mafao na mikopo ya kukuza biashara zao.

“NSSF imeleta furaha katika kikundi chetu kwani katika yale mafao saba yanayotolewa na shirika hilo tumeanza kunufaika na mafao la matibabu,” anasema Richard.

Anasema katika kupunguza gharama za maisha waliamua kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na baadaye katika NSSF, na mpaka sasa wanachama wao 28 wameshajiunga na wameanza kunufaika na mafao ya matibabu.

Richard anasema wanachama wote wa kikundi hicho wameshuhudia wenyewe baada ya kujiunga na NSSF maisha yao yameanza kubadilika kwa sababu wananufaika moja kwa moja na mafao yanayotolewa na shirika hilo.

“NSSF imeleta faraja kubwa katika kikundi chetu, imetuwezesha idadi ya wanachama kuongezeka hili ni jambo la kujivunia sana, tunaviomba vikundi vyengine wajiunge na shirika hili,” anasema katibu wa Kivulini Youth Network.

Naye mkazi wa Kibamba, Joseph Raphael anaishukuru NSSF kwa kupanua huduma zao na kuzisogeza karibu na wananchi na kuwawezesha wananchi wengi kupata elimu ya hifadhi ya jamii pamoja na kujiunga na shirika hilo.

Anasema baada ya kufika katika banda hilo alipatiwa huduma mzuri na tatizo lake limepatiwa ufumbuzi, hivyo aliwashauri wananchi na wanachama wa NSSF kuwa na utamaduni wa kutembelea mabanda ya shirika hilo kila linaposhiriki katika maonesho mbalimbali sehemu mbali mbali nchini.

Kampeni ya One Stop Jawabu ilianza Septemba 14, mwaka huu kwenye Viwanja vya Mbagala Zakhem kwa wiki moja na kisha kuhamia Viwanja vya Temeke Mwembe Yanga, ambako itahitimishwa leo Jumatatu.

Chanzo: habarileo.co.tz