Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NMB yasaidia waathirika wa mafuriko

075500961a740329ea57764b001398e1 NMB yasaidia waathirika wa mafuriko

Tue, 19 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BENKI ya NMB mkoani Mtwara imetoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo chakula kwa waathirika wa mafuriko yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha siku mbili mfululizo mkoani Mtwara.

Msaada huo wenye thamani ya Sh milioni tano ulitolewa katika vituo vya kuhifadhi waathirika hao vya Sino na Rahaleo huku serikali ikiendelea kufanya utaratibu wa kuondoa maji katika makazi yao ili waweze kurejea.

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo, Meneja wa Huduma wa NMB Kanda ya Kusini, Mohammed Fundi, alisema wameamua kutoa msaada huo ili kuwasaidia waathirika hao wakiwamo watoto wadogo pamoja na wanafunzi.

"Tumeamua kutumia hata hiki kidogo kuwasaidia ndugu zetu. Tumewaletea magodoro, mashuka, unga, sukari, mafuta ya kupikia, mchele, sabuni, chumvi na mahitaji mengine ili viwasaidie kwa muda huo wanaposubiri utaratibu mwingine," alisema.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ufukuno katika Wilaya ya Mtwara, Filomena Mgwale, aliishukuru benki hiyo akisema imetoa msaada utakaowasaidia waathirika wakiwamo watoto na wanafunzi waliopoteza makazi yao.

Akizungumzia waathirika waliohifadhiwa Sino, ofisa mtendaji huyo alisema wapo waathirika wapatao 48 kutoka kata za Ufukuni na Magomeni.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, waathirika 15 kati ya hao hawana makazi kabisa baada ya makazi yao kubolewa na mvua na wengine nyumba zao kubolewa upande mmoja na nyingine kuingiwa na maji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurungezi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Ofisa Mazingira wa manispaa hiyo, Masumbuku Mtesigwa, alisema kuna waathirika wa mafuriko zaidi ya 140 waliohifadhiwa katika vituo vitano vilivyopo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Alisema serikali inafanya jitihada kuokoa nyumba za waathirika hao ili warejee katika makazi yao na kuendelea na shughuli za maendeleo.

Alisema kwa sasa serikali inaendelea kufanya tathmini ili kubaini nyumba zilizoharibika kabisa na kuona namna ya kuwasaidia waathirika ili wapate makazi.

Waathirika wa misaada hiyo waliishukuru benki ya NMB kwa msaada na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuwasaidia kwa mahitaji mbalimbali wakati wanasubiri mwongozo kuhusu makazi yao yaliyoharibika na maji.

Mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo, Zuhura Daudi alisema: "Tunaishukuru NMB kwa msaada ambao kwa kweli, utatusaidia sana kuhakikisha watoto wetu wanakuwa salama na wanapata chakula maana hapa tuna watoto, waume zetu na wanafunzi hatuna chochote cha kusema kinaweza kutusaidia."

Chanzo: habarileo.co.tz