BENKI ya NMB imeibuka kuwa mshiriki muhimu katika mchakato wa kuleta mabadiliko chanya kwenye kilimo cha pamba mkoani Simiyu.
Imeelezwa kuwa NMB imekuwa kinara katika Mkakati Maalumu wa Miaka Mitano wa Mapinduzi ya Kilimo cha Pamba mkoani humo ambao pia unahusisha utoaji elimu kwa wakulima na vyama vya ushirika (AMCOS) na kuwasaidia kujiunga na mfumo rasmi wa kifedha nchini.
Akizungumza katika banda la benki hiyo kwenye viwanja vya Nyakabindi kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji maarufu Nanenane lilipotembelewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji), Angela Kairuki jana, Meneja wa Kanda ya Magharibi wa benki hiyo, Sospeter Magese, alisema pia wamesaidia kuziunganisha AMCOS 26 ambazo zinashiriki kwenye programu hiyo maalumu.
Banda hilo lipo kimkakati kuonesha nini kinafanyika kwenye utekelezaji wa Mkakati Maalumu wa Miaka Mitano (2019-2024) wa Mapinduzi ya Kilimo cha Pamba mkoani Simiyu ambao ulizinduliwa rasmi Machi mwaka jana.
Kwa mujibu wa Magese ambaye ni Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi, moja ya ushiriki wao mkubwa katika mkakati huo ni kutoa Sh bilioni 1.9 kwa ajili ya kukarabati maghala ya pamba kwa lengo la kuhakikisha zao hilo linahifadhiwa kisasa na kwa usalama zaidi.
Pia alisema NMB imesaidia kufungua akaunti 86,000 za wakulima wa pamba ingawa kuna changamoto ya matumizi yake kutokana na wanunuzi wengi wa zao hilo kufanya malipo kwa fedha taslimu.
Katika hotuba yake, Waziri Kairuki ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye maonesho hayo wakati anasoma hotuba yake katika viwanja vya Nyakabindi nje kidogo ya Mji wa Bariadi aliagiza malipo yote ya mauzo ya pamba yafanyike kupitia akaunti za benki.