Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NEMC yawaonya wakandarasi wanaosafisha mito Dar

13523 NEMC+PIC TanzaniaWeb

Fri, 24 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Heche Suguta amewaonya wakandarasi wanaosafisha mto Mbezi na matawi yake kutojikita kwenye biashara ya kuuza mchanga na kusahau jukumu lao la msingi.

Kampuni tatu zilizoshinda kandarasi ya kusafisha mto huo kufuatia mafuriko yaliyoyokea Oktoba mwaka jana ni pamoja na Othyblue International, Benson na Carrebean.

Akizungumza katika mkutano ulioitishwa kati ya mitaa ya Mbezi A, Ukwamani na Mzimuni wilayani Kinondoni leo Agosti 23 Heche amesema NEMC itaangalia mkataba wa wakandarasi hao.

"Wengi mmesema kazi iendelee ila kuwe na usimamizi mzuri. Hizi kazi zinafanyika kwa nyaraka, tutaangalia mpango kazi wao. Je, wanafuata sheria? Mbona wanachimba mchanga tu?" amehoji Heche.

Licha ya baadhi ya wananchi kuridhia usafishwaji huo, wamekosoa uchimbaji wa mchanga na kutotekelezwa kwa makubaliano.

"Nia ya serikali kuleta tingatinga ni kusafisha mto, kwa hiyo uchimbaji wa mchanga sasa basi na mchanga uliolundikwa katikati uondolewe," amesema May Maumba ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mzimuni.

Naye Joseph Mfaume amesema licha kazi nzuri zinazofanywa na wakandarasi hao, wananchi wanashindwa kuwaelewa kwa sababu ya kukosa mpango kazi.

Mkandarasi wa kampuni ya Othyblue International, Heri Mohammed amrsema malalamiko ya wananchi hao yana sura ya kisiasa na kiuchumi.

"Wengi wanaopinga kazi hii ni wanachama wa Chadema na wanaounga mkono ni CCM. Halafu kuna watu walikosa tenda ya kazi hii, ndio wanahamasisha wananchi kupinga kazi yetu," amesema Mohammed.

Mwakilishi wa Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu, Mshube Wilson amewataka wananchi hao kupeleka malalamiko yao kwenye kamati ya mazingira ya kata badala ya kuwasumbua wakandarasi wawapo kazini.

Chanzo: mwananchi.co.tz