Kundi la watu wanaodaiwa kua ni Wakazi wa Kijiji cha Maharaka kilichopo Kata ya Doma Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, wamewavamia Wafugaji jamii ya Kimasai wakati wakinywesha mifugo Mtoni kisha kukatakata Ng’ombe 13 na kumjeruhi mfugaji mmoja mkononi.
Wakizungumza mbele ya Wanahabari Wafugaji hao waliokua wakichunga Ng’ombe hao katika mto uliopo kwenye kijiji hicho ambapo walifika kwa lengo la kunywesha maji mifugo yao wamesema tukio hilo limetokea majira ya saa sita mchana agosti 31, 2023 baada ya kundi la watu zaidi ya 30 kuwavamia kisha kuanza kuwapiga na kushambulia mifugo.
Waathiriwa hao wafugaji akiwepo Mbayeni Kipareni na Adam Nduleil ambao walikutwa na mkasa huo wa kupigwa wakisema wakati wananchi hao wakitekeleza tukio hilo walikua wakiwauliza ni kwanini wanaleta mifugo katika mto huo kunywa maji.
Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa Morogoro, ACP Alex Mkama amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema uchunguzi unaendelea kuwabaini waliohusika, huku akitoa onyo kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.