Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee mwenye zaidi ya miaka 80 kibarua wa kuponda kokoto

18281 Pic+kokoto TanzaniaWeb

Thu, 20 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kati ya wanaume wenye bahati ya kuhesabu miaka mingi duniani wakiwa na afya njema ni Mzee Adolph Miyula (81), mkazi wa Kata ya Pasua katika Manispaa ya Moshi.

Licha ya umri mkubwa alionao, mzee huyo anajihusisha na kazi ya kuponda kokoto kupata ridhki ya kila siku. Pamoja na ugumu wa kazi hiyo yenye kipato kidogo, huamka asubuhi na mapema katika jitihada za kuepuka kuwa tegemezi na ombaomba mitaani.

Akizungumza na gazeti hili katika Mtaa wa Kilimani ambako hufanya kibarua cha kugonga mawe, Miyula anaeleza kuwa alizaliwa Sumbawanga Mjini. Enzi za ujana wake anasema alikuwa akifanya kazi kwenye kampuni za ujenzi wa barabara.

Baadaye anasema aliondoka Sumbawanga na kuhamia mkoani Morogoro ambako alikuwa anajihusisha na kilimo hadi mwaka 2012 alipougua na kupooza.

Baada ya kupata tatizo hilo, alichukuliwa na mmoja wa watoto wake anayeishi Kilimanjaro ili amuuguze.

“Niliishi na mwanangu lakini baadae aliolewa na mume wake hakunihitaji hivyo nikachukuliwa na Kanisa la Betheli Matindigani Pasua ambalo limenipangishia nyumba huku mimi nikijihudumia kwa mahitaji mengine ikiwamo chakula na mavazi,” anasema Miyula.

Kugonga kokoto

Anasema baada ya kupangishiwa nyumba, alilazimika kutafuta shughuli ya kufanya ili kuondokana na utegemezi, ambapo alipata kibarua hicho cha kugonga mawe na kila siku asubuhi, huamka mapema kufanya kazi hiyo kuhakikisha siku yake inaenda vyema.

Kwenye kibarua hicho, anasema analipwa kutokana na kokoto anazotengeneza hivyo juhudi zake ndizo kipato chake kila siku.

Miyula anaeleza kuwa kazi hiyo anaifanya kutokana na kukosa mtaji wa kufanya shughuli nyingine licha ya ukweli kwamba mapato anayotengeneza kwa siku ni kidogo sana ambazo mara nyingi huishia kwenye mahitaji madogo madogo hasa chakula na mavazi.

Analeza kuwa, akiponda mawe na kujaza ndoo moja ya lita 20 hulipwa Sh300 na hujitahidi kila siku kujaza ndoo 10 ili alipwa Sh3,000 ambayo huitumia kwa ajili ya kuendesha maisha yake.

“Nikijitahidi sana naweza kujaza ndoo 10. Fedha ninazopata ndizo nazozitumia kukimu maisha yangu kama kula, kuvaa na matumizi mengine kwa kuwa ni ndogo sana ikilinganishwa na hali ya maisha ilivyo kwa sasa,” anasema.

Mzee Miyula anaeleza kuwa, endapo atapata mtaji, anaweza kujiajiri mwenyewe kwa kuagiza mawe yake na kuyaponda ili kukuza kipato chake kwa maelezo kuwa fedha anazookoteza kwa sasa hazitoshelezi matumizi yake.

Ndoo moja ya kokoto ambayo mzee huyo na vibarua wenzake huijaza kwa Sh300 inauzwa kati ya Sh1,200 hadi Sh1,500 kutegemeana msimu ulivyo jambo analoamini akiifanya kwa mtaji wake mwenyewe ataboresha maisha yake.

Afya yake

Akizungumzia afya yake kwa sasa, Mzee Miyula anasema ni njema ingawa mguu mmoja bado unamsumbua na kumfanya atembee kwa shida.

“Kwa sasa afya yangu ni nzuri, ila mguu ndio una shida, umekuwa ukipata ganzi na ndiyo maana mnaniona natembea kwa kuchechemea”anasema.

Mzee Miyula anasema hana bima ya afya kwa kuwa fedha anazopata hazitoshelezi mahitaji yake ya nyumbani na kulipia bima Sh30,000 kwa mwaka.

“Sina bima ya matibabu. Nitapata wapi hela? Kipato changu kidogo, nawezaje kujiunga kwenye bima ambayo ni Sh30,000?” anahoji.

Ushauri kwa vijana

Akiwaasa vijana, Mzee Miyula anasema wengi kwa sasa hawapendi kufanya kazi na wegine huishia kukaa vijiweni huku wakilalamika kukosa ajira wakati baadhi wanachagua kazi za kufanya.

Anasema kazi ya kugonga mawe ina lipa endapo mtu ana mtaji kwa kuwa kila siku watu wanajenga hivyo vijana wanaopenda kujituma wanaweza kujiingiza kwenye kazi hiyo na kuondoka na maisha ya utegemezi kwa familia zao.

Anatumia nafasi hiyo pia kuwashauri kujiunga kwenye vikundi na kuchangamkia fursa za mikopo ambayo imetangazwa na Serikali kupitia halmashauri ili waweze kupata mtaji na kujiajiri wenyewe.

“Kazi hii mtu ukiwa na mtaji na ukajiajiri inalipa. Lori moja la mawe linauzwa Sh90,000 na ukiyaponda na kuyauza unapata faida nzuri. Bei ikiwa nzuri sokoni, unaweza kupata hata mara mbili ya fedha uliyonunulia,” anaeleza Miyula.

Anasema vijana wakiacha kubweteka mitaani na kuchagua kazi na kujiingiza kwenye biashara hiyo, wanaweza kupata fedha ambazo zitawawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na lindi la umaskini.

Anasema vijana wengi wanaiogopa na kuiona kazi hiyo ya kuponda kokoto haifai lakini ni nzuri kama mtu ana mtaji tofauti na kukaa nyumbani ukisubiri usaidiwe kukidhi mahitaji yako.

Wengi wanaoiogopa kazi hiyo, mzee huyo anasema ni wale wanaobweteka mtaani kwa uvivu na kulalamika kukosa ajira huku wengine wakishinda vijiweni na kutafuna mirungi jambo ambalo ni hatari kwa afya.

“Vijana wakijiunga watatu au wanne, mmoja akawa mbanjuaji, mwingine mgongaji kuyapunguza ukubwa na mwingine akawa anayaponda na kuyanga, watapata mtaji na watafanya kazi nzuri ambayo itawainua kiuchumi,” anasema.

Licha ya miaka yake kusogea, mzee huyu anasema hakuna haja kwa mtu yeyote, bila kujali umri wake anasema hakuna haja ya kuomba kwa ndugu bali kujishughulisha.

Kutokana na hali ya uchumi ilivyo, anashauri kilammoja ajishughulishe na vijana waamke na kujituma kwa kufanya kazi bila kuchagua hatua ambayo itawawezesha kujiongezea kipato na kupunguza malalamiko na manung’uniko ambayo huongeza gharama za maisha kwa wengine.

“Huu ni mwaka wa kazi, kubweteka hakusaidii, mtu anakula mirungi anajiingiza kwenye ulevi na utumiaji wa dawa za kulevya halafu anataka achague kazi. Kwa kweli huu si wakati wa kufanya starehe kwani hazina maana na haziwapi tija yoyote katika maisha yao ya leo na hata ya baadaye. Ni lazima wabadilike na kuchukua hatua,” anasema.

Wastaafu

Kutokana na kuongezeka kwa uelewa, watu wengi hupanga lini watastaafu. Huenda si kustaafu bali kuachana na waajiri wao ili wasimamie miradi yao.

Licha ya mipango binafsi, Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeweka ukomo wa mtu kuajiriwa bila kujali hali ya afya yake. Kwa mujibu wa viwango vya kimataifa ambavyo hutumiwa na nchi nyingi duniani ikiwamo Tanzania, hakuna anayepaswa kuajiriwa baada ya kufikisha miaka 60.

Serikali nchini inatoa nafasi kwa yeyote aliyefikisha miaka 55 kustaafu kwa hiyari na akifikisha miaka 60 ni lazima. Katika umri huo, inaelezwa kuwa binadamu anapaswa kutulia na kuacha kukimbizana na ratiba za ofisini.

Makadirio ya Umoja wa Mataifa yanaonyesha mpaka mwaka 2017, kila Mtanzania ana uhakika wa kuishi wastani wa miaka 66.7 ambayo imeongezeka kutoka miaka 64.9 mwaka 2015.

Kwa makadirio hayo ya Umoja wa Mataifa, Mtanzania ana uhakika wa kuishi miaka mitano baada ya kustaafu ingawa wapo wanaoendelea kufaidi pumzi ya Mwenyezi Mungu kwa miaka mingi zaidi. Wachache, waliokuwa kwenye mfumo rasmi nchini, hulipwa pensheni kila mwezi hali ambayo haipo kwa wale wa sekta isiyo rasmi.

Takwimu za Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) zinaonyesha mpaka mwaka 2015/16 kulikuwa na zaidi ya wanachama milioni 2.23 walioongezeka kutoka milioni 2.14 mwaka 2014/15.

Katika kipindi hicho, SSRA inasema: “Wastaafu wanaolipwa pensheni waliongezeka mpaka 126,358 kutoka 112,010 waliokuwapo 2014/15 huku mafao yaliyolipwa yakiongezeka kutoka Sh1.53 trilioni hadi Sh2.93 trilioni.”

Mwaka huu, makadirio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) yanaonyesha Tanzania itafikisha zaidi ya watu milioni 54 ambao wanastahili kunufaika na rasilimali zilizopo. Miongoni mwao, wanawake ni milioni 27.69 na wanaume ni milioni 26.5.

Chanzo: mwananchi.co.tz