Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee aliyevamiwa na kukatwa mkono aomba kujengewa nyumba yenye usalama

62019 Pic+mzee

Mon, 10 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyarutanga mkoani Morogoro, Said Masongela ameiomba Serikali na wadau mbalimbali kumsaidia mkazi wa kijiji hicho, Nasoro Msingili (69) mwenye ualbino na ulemavu wa macho aliyekatwa mkono na watu waliomvamia nyumbani kwake.

Akizungumza baada ya shirika la Under the Same Sun kufika kijijini hapo kutoa elimu ya kuwalinda watu wenye ualbino, mwenyekiti huyo amesema kwa sasa Msigili anaishi katika mazingira hatarishi kutokana na nyumba yake ya nyasi kuwa mbovu na kwamba anaishi na mke wake ambaye ni ajuza.

Masongera amesema msaada unaotolewa na serikali ya kijiji pamoja na wasamaria wema wengine wa kijijini hapo hautoshelezi mahitaji na mara kadhaa mzee huyo amekuwa akilala na njaa na hata kunyeshewa na mvua kutokana na nyumba yake kuvuja.

“Huyu mzee kwa sasa anaishi kwenye mazingira magumu na hatari, nyumba yake si imara hivyo ni rahisi mtu kuvunja na kumvamia, kama serikali ya kijiji tumekuwa tukijitahidi kuwaeleza viongozi, lakini mpaka sasa hakuna msaada wowote alioupata,” amesema Masongela.

Akieleza namna alivyovamiwa na watu na kukatwa mkono mzee huyo mwenye ulemavu amesema kuwa akiwa amelala na mke wake usiku wa manane ghafla alishtuka na kukuta amezingirwa na watu huku wengine wakimshika mkono wa kushoto na alipojaribu kupiga kelele mmoja wa watu hao alimkata mkono na kikimbia nao.

Mzee Msingili amesema kuwa kwa kuwa haoni hakuweza kuwatambua watu hao hata hivyo baada ya kupata fahamu akiwa hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro aliambiwa kwamba watuhumiwa waliomkata mkono wamekamatwa japokuwa mpaka sasa hajua kesi hiyo imefikia wapi kwa kuwa hajawahi kuitwa mahakamani, polisi wala kwa kiongozi yoyote.

Pia Soma

Akizungumzia hali ya maisha wanayoishi mke wa mzee Msingili, Regina Alphonce amesema kuwa wanakabiliwa na njaa kwa kuwa hawawezi kulima lakini pia nyumba yao sio imara hivyo bado wako hatarini kuvamiwa na kufanyiwa vitendo vya kikatili.

Ofisa mlaghibishi kutoka shirika la kimataifa la Under the Same Sun, Kondo Sefu amesema kwa sasa wanaendesha programu ya kutoa elimu kwa jamii kwa njia ya sanaa ya kuwalinda, kuwatetea na kuwapa haki zao kama watu wenye ualbino.

Mwisho.  

Chanzo: mwananchi.co.tz