Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwili wakwama mochwari siku saba kisa mvutano wa mke na ndugu wa marehemu

37749 Pic+mwili Mwili wakwama mochwari siku saba kisa mvutano wa mke na ndugu wa marehemu

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mwili wa mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Mererani, Jubilate Ulomi umekwama kuzikwa kwa siku ya saba hadi jana baada ya mke wa marehemu na watoto wake kuingia katika mgogoro na ndugu wa marehemu.

Mwili wa mchimbaji huyo anayemiliki migodi Mererani, umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Wilaya Hai kusubiri uamuzi wa Mahakama au muafaka baina ya familia ya mke na mume.

Akizungumza na Mwananchi jana, mke wa marehemu, Zainabu Rashid alisema yeye na wanaye wawili wanapinga kuzikwa mwili huo kutokana na baadhi ya ndugu kutotaka kufanyika uchunguzi wa kifo hicho huku wakimtenga na msiba huo.

Zainabu alisema kwamba alipata taarifa kuwa mumewe alifariki Jumanne iliyopoita huko Nairobi, Kenya kwa kuumwa lakini alisema hawakumpa taarifa yeye wala watoto wake juu ya kuugua. Alisema Alhamisi iliyopita, shemeji yake aliyekuwa na marehemu alimtaka awapeleke watoto kwa Sadala wilayani Hai ili wakazike.

Hata hivyo, alidai kuwa shemeji yake huyo alimweleza kuwa hatakiwi kwenda msibani kwani kabla ya mume wake kufariki dunia walikuwa na ugomvi.

Alisema licha ya ukweli kuwa kwa miezi sita walikuwa hawaishi na mumewe kutokana na mgogoro wa kifamilia, hawakuwa wameachana na wameishi pamoja kwa miaka 12 hivyo ana haki ya kumzika.

“Baada ya kifo cha mume wangu wameingia ndani na kuvunja selfu na kuchukua mali mbalimbali zikiwamo bastola mbili bila kunishirikisha. Wameeleza kuwa vitu vimepelekwa Machame nyumbani kwa wazazi wa mume wangu” alisema.

Alisema kutokana na mgogoro huo wamemuomba mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya kuingilia kati ili haki yake na watoto ipatikane ikiwamo kupata heshima kuaga mwili wa mumewe.

Akizungumzia mgogoro huo baada ya kusikiliza pande zote, Ole Sabaya aliagiza suala hilo kufikishwa mahakamani.

“Nimesikiliza pande zote. Huu ni mgogoro wa kisheria, nawashauri suala hili lipelekwe mahakamani kwani mke ana haki kumzika mume wake na haki nyingine,” alisema.

Julius Jubilate ambaye ni mtoto mkubwa wa marehemu alisema amebaini kwamba kuna mkakati wa kunyimwa haki zake.

“Sikujua kama baba alikuwa anaumwa nilipigiwa simu nikiwa chuoni niende Kwa Sadala (Hai) ili wanipeleke msibani” alisema Julius anayesoma katika Chuo cha Uhasibu Arusha.

Alisema anachokitaka ni baadhi ya ndugu wa familia kuacha njama za kuwanyima haki yeye, mama yake mdogo na wadogozake.

Agness Mollel ambaye ni mama mdogo wa mke wa marehemu, aliiomba Serikali kuingilia kati ili haki ipatikane.

“Wanataka kuzika bila kujua haki ya mkewe na watoto. Nyumba wamefunga, magari na mali zote wamepeleka Machame bila kumshirikisha mke wa marehemu” alisema.

Alisema katika hali ya utata tayari wanafamilia wamemteua mdogo wa marehemu kusimamia mirathi bila kumshirikisha mkewe.

Ndugu wa marehemu, Werandumi Ulomi alipoulizwa kuhusu mgogoro huo hakutaka kuzungumza na badala yake alitaka suala hilo kuachwa kwa wanafamilia.



Chanzo: mwananchi.co.tz