Wakazi wa Mtaa wa Buyekera katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, wamekumbwa na taharuki baada ya kuona mwili wa kichanga ukielea katika mto Kanoni.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa wakiwa wanapita katika eneo hilo, waliona mwili wa kichanga hicho ambacho kikiwa kimefariki na mwili wake ukielea na kulaani kitendo hicho, huku wakiomba uchunguzi ufanyike kumbaini aliyehusika ili achukuliwe hatua.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Buyekera lilipotokea tukio hilo Justini Kamugisha, amesikitishwa na kitendo hicho na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika pindi wanapobaini wahusika wa vitendo hivyo.
Akizungumza na EATV Mkuu wa kikosi cha Zimamoto na uokoaji Mkoa wa Kagera Hamis Dawa, amesema kuwa walipata taarifa kutoka kwa wananchi juu ya kuonekana kwa kichanga hicho katika maji ya mto huo na kulazimika kwenda kuopoa mwili wake.