Arumeru. Mamia ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro na kata ya Mbuguni wilayani Arumeru, jana saa 3 usiku wameupokea mwili wa mmiliki wa mgodi wa madini ya Tanzanite, marehemu Thomas Mollel maarufu kama Askofu.
Mwili huo ulipokelewa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (Kia) na kuufikisha nyumbani kwake kata ya Mbuguni saa 6 usiku.
Marehemu Mollel alifariki dunia Mei 20 mwaka huu jijini Dodoma alipokwenda bungeni kumsindikiza kuapishwa mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki, John Palangyo.
Akizungumza na MCL Digital leo Jumatatu Mei 27, 2019 Katibu wa CCM wilaya ya Meru, Shabani Mdoe amesema mwili wa marehemu Mollel ulipopelewa Kia jana saa 3 usiku na kufikishwa saa 6 usiku nyumbani kwake Mbuguni.
Mdoe amesema mwili wa marehemu Mollel ulichelewa kufika Kia baada ya ndege iliyombeba kutoka jijini Dodoma, kupitia Dar es salaam na Zanzibar na kufika Kia.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mbuguni, Willy Melanyi, amesema wakazi wa eneo hilo wamepata pigo kubwa kwani marehemu Mollel alikuwa mtu mwenye mapenzi mema na wananchi wa eneo hilo.
Pia Soma
- MADAI: DPP awatuhumu wabunge kwa rushwa, Spika ajibu
- UCHOKOZI WA EDO: ‘Sauzi’ kutamuachia maswali mengi Namba Moja
- Mwakilishi apinga vijana kusaidiwa mahari ili waoe
Mkazi wa Boma Kubwa kata ya Mbuguni, Hamis Amry amesema marehemu Mollel alikuwa mzee wa kuigwa na wananchi na vijiji vya Kikuletwa, Mikungani, Komolo na Mbuguni, wamepata pigo kubwa.
Amry amesema wachimbaji madini wamepata pigo kubwa kwani Mollel alikuwa anasaidia mno wachimbaji wenzake ambao hawakuzalisha madini.
Mchimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mirerani, Haji Msham Ngokwe amesema sekta ya madini imepoteza mtu muhimu kwani Mollel ni miongoni mwa matajiri wa mwanzo mwanzo kupata madini ya Tanzanite.
"Huyu alikuwa na roho nzuri hadi watu wakamuita Askofu kutokana na kuwa na roho ya utoaji," amesema Ngokwe.