Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwili wa Frank Kapange watimiza siku 206 mochwari

33645 Frank+pic Tanzania Web Photo

Thu, 27 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Ikiwa imepita miezi sita na siku 22 ambazo ni sawa na siku 206, mwili wa marehemu Frank Kapange (22) unaendelea kuhifadhiwa mochwari katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya huku kukiwa hakuna dalili za kuzikwa siku za karibuni.

Frank alifariki dunia Juni 4 ambapo kifo chake kiligubikwa na utata baada ya ndugu kudai kuwa kilitokana na kipigo akiwa mikononi mwa polisi.

Kijana huyo alikuwa mfanyabiashara wa nguo za mitumba katika Soko la Sido jijini hapa.

Kufuatia madai hayo, ndugu waligoma kuchukua mwili wake kwa ajili ya maziko wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusiana na kifo.

Ili kukazia msimamo wao, ndugu hao walikimbilia mahakamani kufungua kesi kuiomba itoe amri ya kufanyika kwa uchunguzi wa kitabibu wa kifo.

Hata hivyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ilitupilia mbali shauri hilo na kuamuru mwili huo uzikwe na ndugu hao na pia wabebe gharama zote ikiwamo za kuuhifadhi chumba cha maiti.

Ndugu hao walidai kutoridhishwa na uamuzi huo, hivyo waliamua kukata rufani Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo nayo ilitoa uamuzi wa kufuta kesi hiyo baada ya kuridhika kwamba mlalamikaji hakufuata taratibu zilizopaswa wakati wa kuifungua.

Msemaji wa familia ya marehemu, Julius Kapange aliliambia Mwananchi jana kwamba ndugu wamekubaliana kuuchukua mwili wa ndugu yao ili wauzike kwa sababu sehemu waliyokimbilia kutafuta haki hawajafanikiwa, lakini bado mwenye uamuzi wa mwisho ni wakili wa familia, Moris Mwamwenda.

Julius alisema, “Tangu siku tulipompa msimamo wa kifamilia alituambia tumsubiri anakuja Desemba 5, lakini hadi sasa hajafika.”

“Tumejaribu kumtafuta tena juzi (lakini) ameonekana kutoridhika na msimamo wetu, hivyo tumeamua tumuachie atalimaliza mwenyewe.

Alisisitiza kuwa, “Hatuwezi kulazimisha, yeye (wakili wetu) ndiye aliyekuwa anasimamia kila kitu, hata tukisema tunakwenda kuuchukua mwili bado yeye ndiye atakayehusika kwa kila kitu.”

Wakili wa familia

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Wakili Mwamwenda hakupatikana baada ya simu yake kutokuwa hewani.

Hata hivyo, Desemba 11, Mwananchi lilizungumza naye na akatoa msimamo wake.

Alisema tayari ameshaandika maombi ya kukata rufani Mahakama ya Rufaa na suala hilo liko kisheria zaidi.

“Ndugu wanaopenda kijana wao akazikwe wamekata tamaa,” alisema wakili huyo.

“Tunachokitaka sisi ni kufanyika kwa uchunguzi rasmi wa kisheria wa kifo chake, hakijulikani kimesababishwa na nini. Ninakwenda Mahakama ya Rufaa ambako ninajua itatoa mwongozo nini kifanyike, nina imani nitashinda kesi hii.”

Mwamwenda alisema haangalii ni muda gani mwili wa marehemu umekaa mochwari wala suala la gharama, bali ni haki itendeke na jamii ijue.

Pia, alisema haki wanayoitaka itakapojulikana anapenda wahusika wa tukio hilo wakibainika wachukuliwe hatua za kisheria.

Ushauri wa polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei aliishauri familia hiyo kwenda kuuchukua mwili wa kijana huyo na kuuzika, badala ya kuendelea kuuacha mochwari huku gharama za kuuhifadhi zikiongezeka.

Kamanda Matei alisema kuendelea kuuacha ni kutomtendea haki marehemu na si utamaduni wa Kiafrika.

Alisema: “Madai yao hayana msingi, ndiyo maana mahakama zote mbili ziliyatupilia mbali, lakini siku moja mama wa kijana huyo (marehemu) alikuja ofisini kwangu akaniomba kumzika mtoto wake na mimi nikasema waseme wanachohitaji nitawasaidia.”

Gharama za kuhifadhi

Mwili huo umekaa hospitalini hapo kwa siku 206 hadi jana na gharama za kuuhifadhi kwa siku moja ni Sh20,000, hivyo hadi sasa zimefikia Sh4.12 milioni.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Petro Sema alisema wanaendelea kuutunza mwili huo na ndugu wakishamaliza masuala yao ya mahakamani, watakaa nao mezani kufanya mazungumzo juu ya ulipaji wa gharama.



Chanzo: mwananchi.co.tz