Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwili wa Frank Kapange wafikisha miezi saba mochwari

Sat, 5 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Mwili wa Frank Kapange (21), umetimiza miezi saba na siku mbili ukiwa mochwari, baada ya ndugu kugoma kuuchukua wakitaka uchunguzi dhidi ya kifo chake ufanyike.

Wakati mwili huo ukifikisha muda ambao ni sawa na siku 215 ukiwa chumba cha kuhifadhia maiti, wakili wa familia yake, Moris Mwamwenda amesisitiza kuwa alishakata rufani Mahakama ya Rufaa na sasa anasubiri majibu ya rufani yake.

Frank alifariki dunia Juni 4, mwaka jana ambapo kifo chake kiligubikwa na utata baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa mfanyabiashara wa nguo za mitumba katika Soko la Sido jijini hapa aliuawa kwa kipigo akiwa mikononi mwa polisi.

Kutokana na madai hayo, ndugu hao waligoma kuchukua mwili kwa ajili ya kuzika wakitaka kujiridhisha na sababu za kifo chake, ambapo walifungua kesi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya wakiiomba kutoa amri ya kufanyika kwa uchunguzi.

Mahakama hiyo chini ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Michael Mteite ilitupilia mbali shauri hilo na kuamuru mwili huo uzikwe na ndugu wabebe gharama zote za mazishi.

Baada ya hukumu hiyo, ndugu hao walidai kutoridhika na uamuzi huo wakaamua kukata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo nayo ilitoa uamuzi wa kufuta kesi hiyo baada ya kuridhika kwamba mlalamikaji hakufuata taratibu zilizopaswa wakati wa kuifungua.

Wakili wa familia

Akizungumza na Mwananchi jana, Wakili Mwamwenda alisema baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa kufuta shauri hilo hakuridhika, hivyo alikata rufani Mahakama ya Rufaa.Alisema kwa sasa anachosubiri ni kuitwa na msajili wa mahakama hiyo ili kujulishwa kama shauri hilo limeshafanyiwa kazi.

“Notisi ya kukata rufani nilishaiwasilisha kwa msajili, hivyo inashughulikiwa huko,” alisema.

“Ninachosubiri ni kuambiwa nipeleke sababu za rufaa. Suala hili halipo kwangu tu kwa sasa, bali na kwa msajili ambaye anashughulikia.”

Awali, msemaji wa familia hiyo, Julius Kapange aliliambia Mwananchi baada ya mahakama zote mbili kutupilia mbali shauri lao kuwa wametafakari na kuamua kwenda kuuchukua mwili wa ndugu yao ili wauzike, lakini wakili wao (Mwamwenda) amewazuia kutekeleza hilo.

Polisi, hospitali

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei aliishauri familia hiyo kwenda kuuchukua mwili huo na kuuzika badala ya kuendelea kuuacha mochwari huku gharama za kuuhifadhi zikizidi kuongezeka.

Kamanda Matei alisema kuendelea kuuacha mwili wa kijana huyo mochwari ni kutomtendea haki marehemu, na ni vyema ndugu wakauheshimu kwa kuuchukua na kwenda kuuzika.

“Kwanza madai yao hayana msingi, ndio maana mahakama zote mbili ziliyatupilia mbali, lakini siku moja mama wa kijana huyo (marehemu) alikuja ofisini kwangu akaniomba kumzika mtoto wake, na mimi nikasema waseme wanachohitaji nitawasaidia,” alisema Matei.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Petro Seme alisema jana kwamba, bado wanaendelea kuuhifadhi mwili wa kijana huyo huku wakisubiri uamuzi wa kisheria utakaotolewa na pia maelekezo tofauti.

Gharama za kuhifadhi

Gharama za kuhifadhi mwili wa marehemu hospitalini hapo ni Sh20,000 kwa siku.

Kwa maana hiyo mwili wa Frank uliotimiza siku 215 hadi jana unatakiwa kulipiwa Sh4.2 milioni.



Chanzo: mwananchi.co.tz