Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwili uliosuswa na ndugu mochwari kwa siku 178 wasubiri wakili

29364 Mwili+pic TanzaniaWeb

Thu, 29 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Familia ya marehemu Frank Kapange aliyetimiza siku ya 178 mwili wake ukiwa chumba cha kuhifadhia maiti imesema hatima ya kuendelea na kesi ipo mikononi mwa wakili, Moris Mwamwenda.

Frank alifariki dunia Juni 4 mwaka huu huku kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana huyo aliyekuwa akifanya biashara ya mitumba soko la Sido jijini hapa alifariki kwa kipigo akiwa mikononi mwa polisi jijini Mbeya.

Ndugu hao waligoma kuuchukua mwili na hadi jana ulikuwa chumba cha kuhifadhia maiti ingawa tayari baadhi wameanza kukubali kuchukua mwili huo kwa ajili ya mazishi.

Agosti 24 mwaka huu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite aliamuru mwili wa Frank kuchukuliwa na ndugu kwa ajili ya mazishi.

Ilikuwa baada ya kutupilia mbali maombi ya familia ya kuiomba mahakama hiyo iamuru kufanyika kwa uchunguzi wa kiini cha kifo cha Frank baada ya kuridhika na mapingamizi yaliyowasilishwa na mawikili wa upande wa Serikali.

Hata hivyo, ndugu hao walidai kutoridhika na uamuzi huo hivyo wakaamua kukataa rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo nayo ilitoa uamuzi wake wa kuifuta kesi hiyo baada ya kujiridhisha kwamba mlalamikaji hakufuata taratibu zilizopaswa wakati wa kufungua kesi hiyo.

Akizungumza jana na Mwananchi, Julius Kapange ambaye ni msemaji wa familia ya Kapange alisema ndugu wengi wameamua kukubali matokeo na kutaka kuuchukua mwili wa kijana wao ili wakauzike, lakini hawawezi kufanya hivyo hadi watakapomsikiliza wakili wao kwanza.

“Suala letu bado lipo pale pale, na sasa tunamsubiri tu wakili, amesema atakuja tarehe 5 mwezi ujao ndio tutakaa kifamilia kumsikiliza msimamo wake, lakini tulio wengi tunaona bora tukauchukue tu mwili wa kijana wetu, kwani tulikotegemea kupata haki yetu (mahakamani) waliamua kutoa uamuzi ambao hatukuridhika nao”.

Wakati Kapange akitoa msimamo wa familia, wafanyabiashara waliokuwa wakiuza mitumba na marehemu Frank katika Soko la Sido walionekana kusikitishwa na kitendo cha Mahakama kutoa uamuzi ambao hawakuridhika nao. Walisema ni jambo la ajabu na la kusikitisha mwili wa marehemu kukaa mochwari muda wote huo na kutaka utaratibu wa kisheria ufanyike haraka ili wakamzike mwenzao.

Mfanyabiashara wa mitumba wa Sido, Emmanuel Mwaifwani alisema anashindwa kuelewa nini kinaendelea kwa polisi na Serikali akidai kuna kitu hakiko sawa kwa upande wa utoaji haki

“Naona kuna mahali hapajakaa vizuri kwamba sheria kama hauijui vizuri inakuacha upotee jambo linalosababisha kurudiarudia mambo,” alisema Mwaifwani.

Smati Mwaipungu ambaye pia ni mfanyabiashara wa mitumba sokoni hapo, alisema chumba alichokuwa akifanyia biashara marehemu Frank hakijafunguliwa tangu alipokifunga mwenyewe kabla ya kukutwa na umauti.

Gerald Aile, ambaye ni rafiki wa marehemu, alimuelezea kuwa alikuwa mstaarabu, asiye na matatizo na aliyekuwa akifanya biashara zake kama wengine na kwa ushirikiano.

Soma zaidi:

Mwili wa Frank waendelea kusota mochwari



Chanzo: mwananchi.co.tz