Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenyekiti wa mtaa apigwa risasi

RISASI 2222222222 Mwenyekiti wa mtaa apigwa risasi

Sun, 30 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Mtaa wa Shanwe uliopo Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Mustafa Kimasa amenusurika kifo, baada ya kudaiwa kupigwa risasi maeneo mbalimbali ya mwili wake na watu wasiojulikana, huku chanzo kikihisiwa ni mgogoro wa ardhi.

Akizungumza akiwa katika hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi akipatiwa matibabu, Mwenyekiti huyo amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Oktoba 29,2022, akiwa nyumbani kwake amelala, ndipo alisikia mlango ukigongwa.

Kimasa amesema mtu aliyekuwa akigonga mlango ni mmoja na alikua akimtaka atoke kumsadia ana shida, wakati akijiandaa kutoka akasikia akisema: ” Toka nikumalize nimetumwa roho yako,”amesema Kimasa.

Kwa upande wake, mke wa Mwenyekiti huyo, Zubeda Abdallah, akisimulia tukio hilo amesema mtu huyo aligonga mlango mara tatu, kisha kuanza kupiga risasi mlangoni.

“Hakuingia ndani aliishia mlangoni baada ya mume wangu kufungua mlango akampiga risasi wakati akiondoka alisema na bado tutakukomesha taarifa zako tumeishazipata,”amesema Zubeda.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Shanwe, Fadhil Makolokolo, amesema mtu huyo kipindi anaondoka katika eneo hilo alidondosha karatasi yenye majina ya watu waliotakiwa kuuawa, huku akidai na jina lake likiwemo.

“Sasa tunahisi chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi katika shule ya msingi Shanwe, eneo hilo lina mgogoro miaka 10 sasa,  maana ile ordha ya majina inamtaja Mwenyekiti wa Mtaa, inanitaka mimi, Mtendaji wa kata, Mkuu wa shule ile tuko kama watano hivi.

“Sasa wote wale tupo kwenye ule mgogoro na huo mgogoro hadi DC anaujua na juzi tu alikuja kufanya mkutano ikasemekana kesi ya huo mgogoro ianze upya,”amesema Makolokolo.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Michael Ndaile, amesema alipigiwa simu na mwananchi wake akijulishwa kuwa Mwenyekiti amepigwa risasi, ila kuna karatasi ya majina ya watu waliotakiwa kuuawa na yeye akiwemo.

“Nilipigiwa simu sio kwamba kwa ajili ya tukio, ila ilinitaka nijihami kwa sababu na mimi nimetajwa, kwanza alituma meseji sikuelewa nikampigia simu akasema meseji inavyosema ndio hivyo,”amesema Ndaile.

Naye Boniphace Lyimo, ambaye ni Katibu hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi, amekiri kumpokea mgonjwa huyo na kudai kuwa kuna baadhi ya risasi zimebaki katika mwili wake, hivyo wapo katika harakati za kumfanyia upasuaji, ili kuziondoa.

Kwa upande wake Kamanda Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame, amekiri kulifahamu tukio hilo na bado wanaendelea na uchunguzi mara baada ya kukamilisha, taarifa rasmi itatolewa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live